×

Wanasheria Kutoa Misaada kwa Wananchi Mkoani Dar es Salaam

makonda-1Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akiongea na wanasheria na wanahabari ofisini kwake leo.

makonda-2

…Akisisitiza jambo katika hafla hiyo.

makonda-3

Baadhi ya wanasheria waliokuwa katika hafla hiyo.

makonda-4

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyamiva, akitoa ‘neno’ katika mkutano huo.

makonda-5

Makonda akisalimiana na baadhi ya wanasheria.

Na Hilaly Daud

SERIKALI mkoani Dar es Salaam imeamua kupeleka wanasheria vijana sehemu mbalimbali za wilaya zake ili kujitolea kuwasaidia wananchi katika masuala mbalimbali ya kisheria.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakati akizungumza na wanahabari mbele ya wanasheria waliomaliza kozi zao katika vyuo mbalimbali nchini.

Makonda alisema kutoelewa mambo ya sheria kumekuwa changamoto kubwa kwa jamii, hali inayosababisha wananchi kukosa haki zao na kusababisha mlundikano wa kesi mahakamani.

Aliongeza kwamba miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na malalamiko ya rushwa dhidi ya vyombo vinavyotoa haki, ucheleweshwaji wa kesi mahakamani, migogoro ya ardhi, migogoro ya ndoa, mirathi na waajiri kuwaachisha kazi waajiriwa bila kufuata taratibu.

Akiwaagiza wanasheria hao, alisema wanatakiwa kutoa msaada wa kisheria kwa watu na makundi ya watu wasio na uwezo katika mashauri ya madai ya jinai, kushughulikia malalamiko mbalimbali juu ya utoaji haki kutoka kwa wananchi na kuwaelimisha kuwaelekeza mahali wanapotakiwa kwenda ili kupata haki zao.

“Miongoni mwa mambo mnayotakiwa kuyafanya ni pamoja na kuandika nyaraka tofauti za kisheria kama vile za wosia, mikataba na kutoa msaada kwa njia ya simu, ’’ alisisitiza Makonda
Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyamiva, katika hafla hiyo, alisema suala la uandikaji wa mirathi ni changamoto kubwa kwa jamii, hivyo ni vyema wananchi wakapata msaada huo wa kisheria ili kupunguza matatizo yanayotokana na jambo hilo.