The House of Favourite Newspapers

Matatizo ya nguvu za kiume!

unhappy-young-couple-sitting-on-bedMatatizo haya ya nguvu za kiume humuathiri mwanaume  na mwanamke  kwa  ujumla. Tatizo  hili   hulalamikiwa  aidha  na  mwanaume  mwenyewe  au  mwanamke  kwa kutofikishwa  kileleni  na  kutofurahia  tendo  la  ndoa, hasa  kwa wale walio katika mahusiano.

Zipo  sababu  nyingi    kama  tutakavyokuja kuona  lakini  matatizo  haya humuathiri  mtu  zaidi  kisaikolojia anapohisi  anashindwa  kutimiza  wajibu  wake au mwanamke kujihisi hapati haki yake ya kufurahia tendo. Mtu   anaweza  kuwa  na  tatizo  dogo  ambalo  kama  ni  mshtuko  na  anapopata  mshtuko  huo  hujikuta  tatizo  linazidi  hivyo  kujikuta  mgonjwa  yaani ana tatizo.

Kwa hiyo  ni  vema  unapotokewa  na  tatizo  hili  usikimbilie  kutumia  dawa  hasa  za  asili  na hata  za  madukani  bali  waone  madaktari  wakufanyie  uchunguzi  katika  hospitali  kubwa.

JINSI TATIZO LINAVYOGAWANYIKA

Tatizo  la  nguvu  za  kiume  limegawanyika  katika   makundi mawili;  Kwanza  ni  tatizo  la  kuzidi kwa  nguvu  za  kiume.

Watu  wengi wamezoea  ukisema  tatizo  la  nguvu  za  kiume ni  upungufu,  lakini  lipo hili  la  kuzidi  isivyo  kawaida  na  kujikuta  mtu  anashindwa  kufikia mwisho au mshindo,  hali  hii  tutakuja  kuiona  kwa  undani.

Tatizo  la  pili  ni  upungufu  wa  nguvu, hili  ndilo  tatizo  lililozoeleka  sana  miongoni  mwa wanaume  wengi.  Upungufu  wa  nguvu za kiume unaweza  kuwa  mdogo  au mkubwa,  nao  una sababu  zake  tutakuja  kuziona.

KUZIDI KWA NGUVU ZA KIUME

Hali  hii  kitaalamu  inaitwa  ‘Painful  Abnormal  Erection  of  The  Penis’.  Mwanaume  mwenye hali  hii  hulalamika  maumivu  makali  ya  uume pale  unaposimama  na  hushindwa  kumaliza tendo. Hali  hii  inaweza  kuwa ya muda  tu  au  ikatokea  mara  moja  moja  na  wakati  mwingine  inaweza  kuendelea  kwa  muda  mrefu.

Chanzo  cha tatizo hili  ni  matatizo  au  magonjwa   ya  mfumo  wa  fahamu,  kulazimisha   uume usimame  kwa  kutumia  madawa  au  njia  yoyote  ile,  uwepo  wa  mawe  katika  kibofu  cha mkojo, maambukizi  katika  njia  ya mkojo, maambukizi  ya tezi dume,  kuziba  kwa  mishipa  ya damu  ya  vena  inayotoa  damu  kwenye  uume  kurudisha  mwilini,  na  hii  huwatokea  zaidi wagonjwa  wa  siko  seli.

Pia matatizo  ya  mfumo  wa  damu  hasa  yanayoambatana  na  kansa  ya damu  au  magonjwa  yanayoathiri  mfumo  wa  damu.

MATIBABU

Tiba  sahihi  ya  tatizo  hili  ni  kutafuta  chanzo  cha tatizo  la  uume  kusimama   kwa  muda mrefu  hadi  mtu  anapata  maumivu. Endapo  hali  kama  hii  inatokea, basi  epuka  kuvaa  nguo za  kubana  au  nguo  za  ndani, jifunge tu shuka  au  msuli na  endapo  utavaa  nguo  kama suruali  au  bukta  basi  hakikisha  uume  unauzungushia  pamba  ya  kutosha, yaani  usikwaruze  kwenye  nguo  ngumu  na  ikaleta  kikwazo  kitachoongeza  maumivu.

 Mgonjwa  apelekwe  haraka  hospitali  ambapo  atapatiwa   matibabu.  Wengi   hutokewa  na hali   hii   kwa   kutumia   dawa   za   kuongeza   nguvu   za   kiume   bila   ya   ushauri wa daktari.

 

UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME ‘IMPOTENCE’

Hali hii huitwa ukhanithi, hapa mtu anashindwa kabisa kufanya tendo la ndoa kwa kutokuwa na uwezo, nguvu zinapungua sana au zinakuwa zimekwisha kabisa.

Upungufu wa nguvu za kiume hutofautiana  na ugumba. Katika suala la ugumba mwanaume huwa hawezi kumpa mwanamke  mimba  kwani  mbegu  zake za  kiume  huwa  hazina  ubora.

CHANZO CHA TATIZO

Tatizo  hili  limegawanyika  katika  makundi au sehemu kuu mbili kitaalamu. Kwanza ni tatizo la upungufu wa nguvu za kiume la  muda  mfupi  na  pili  ni  tatizo  la kudumu.

Aina  hizi  mbili  huweza  kumtokea  mwanaume  yoyote lakini hili  la  muda  mfupi  humtokea mtu  yeyote  kutokana  na  hali  ya maisha ya kawaida kwani  si kila  siku  mtu  anakuwa  sawa. Majukumu  ya  kila   siku yanaweza  kukufanya  ukapoteza  hamu na  usiweze  kuwa  na nguvu za kutosha kwa wakati fulani.

 Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.