MAREKANI: Mwanaanga wa Marekani Gene Cernan, aliyekuwa binadamu wa mwisho kutembea kwenye Mwezi, amefariki dunia akiwa na miaka 82.
Shirika la Anga za Juu la Marekani Nasa limesema limehuzunishwa sana kumpoteza mwanaanga huyo mstaafu.
Cernan alikuwa mmoja wa watu watatu pekee waliowahi kwenda Mwezini mara tatu na ndiye binadamu aliyetembea mwezini mara ya mwisho kabisa, mwaka 1972.
Maneno yake ya mwisho aliyoyasema kabla ya kuondoka kwenye Mwezi yalikuwa: “Tunaondoka jinsi tulivyokuja na, Mungu akitujalia, tutarejea na amani na matumaini kwa binadamu wote.”
Alikuwa kamanda wa chombo cha anga za juu cha Apollo 17 wakati huo.
Ni watu 12 pekee waliowahi kutembea kwenye Mwezi, na kati yao ni sita pekee ambao bado wako hai.
Bwana Cernan ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 82, siku zote aliwasisitiza vijana kufika mwezini ili wasimuache yeye pekee kubakia na sifa hiyo.
Comments are closed.