
Kutoka kushoto ni Meneja wa Sauti za Busara, Ramadhan Journey, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud, Mwenyekiti wa Bodi wa Tamasha hilo, Simai Said na Balozi wa Norway hapa nchini, Hanne Marie Kaarstad.

Balozi wa Norway hapa nchi, Hanne Marie Kaarstad (kulia) akizungumza jambo kwenye mkutano huo.

Wanahabari wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kikiendelea.
Na Denis Mtima/GPL
WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha kubwa la Sauti za Busara linalotarajiwa kufanyika Februari 9-12 mwaka huu Visiwani Zanzibar likitakalowakutanisha wasanii zaidi ya 400 wa vikundi 40 vya muziki kutoka Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud, alisema watu wajitokeze kwa wingi kupata vionjo vya muziki wa asili kutoka kwa wasanii mbalimbari barani Afrika kwani watapatiwa burudani za kiwango kikubwa.
“Zanzibar itakuwa kwenye shamrashamara na mikusanyiko mikubwa ya wageni mbalimbali kwenye hoteli mbalimbali ambapo pia watanufaika na ujio wa wageni kutoka sehemu mbalimbali na baadhi ya wafanyabiashara watanufaika na wageni hao kibiashara,” alisema Yusuf Mahmoud.
Kauli-mbiu ya tamasha hilo mwaka huu ni “Africa United” okiwa na maana kuwa muziki unaunganisha mtu na mtu, moyo na moyo ambapo katika dunia inayozidi kugawanyika, lugha ya muziki inahamasisha umoja na urafiki na mshikamano kwenye mipaka ya walimwengu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha la Sauti za Busara, Simai Said, amewashukuru wadau wote kwa kuendelea kuliunga mkono tamasha hilo akisema uwepo wake unaendelea kusaidia fursa za kiuchumi na kuinua tamaduni za kiafrika duniani.
“Tunaishukuru serikali, mabalozi na wadau wengine kutuunga mkono na kufanikisha tamasha hili kubwa zaidi barani Afrika lakini tunapata changamoto hasa kwa kuwapata wafanyabiashara kuja kuwekeza kwenye tamasha letu la Sauti za Busara hivyo tunaomba wadau kujitokeza kudhamini tamasha hili,” alisema.
Aidha amemwomba Rais John Magufuli kutembelea tamasha hilo siku hiyo ili kujionea namna vijana na wananchi wake wanavyoitangaza Tanzania katika mipaka tofauti na kuvutia fursa za kiuchumi.
Wakati huohuo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne Marie Kaarstad, ambaye nchi yake ni wadhamini wakuu na wa muda mrefu wa tamasha hilo, amepongeza juhudi za uongozi wa Sauti za Busara za kuinua utamaduni wa Mtanzania na tamaduni za Kiafrika kupitia sanaa za muziki unaowakutanisha watu wote na kufurahia ala hizo za muziki, na ahaahidi kuendelea kutoa sapoti.
Meneja wa tamasha la Sauti za Busara, Ramadhan Journey, amesema wasanii wote watatumbuiza moja kwa moja jukwaani hivyo kulifanya tamasha hilo kuwa la kipekee na tofauti kwani huonyesha uhalisia na ufanisi wa hali ya juu.
Kipaumbele cha tamasha hilo ni kuhakikisha kila shabiki anamudu kiingilio hivyo kwa Watanzania watalipa Sh. 6,000 kwa siku na kwa tamasha zima la siku nne watalipa Sh. 20,000.
Aliwataja baadhi ya wasanii watakaoshiriki kwenye tamasha hilo kuwa ni : Freshlyground (Afrika Kusini), Rocky Dawuni (Ghana), Sarabi (Kenya), Pat Thomas na Kwashibu Area Band (Ghana), Simba na Milton Gulli (Msumbiji), Jagwa Music (Tanzania), Bob Maghreb (Morocco), Karyna Gomes (Guinea Bissau) na Sami Dan and Zewd Band (Ethiopia), Chibite Zawose Family (Tanzania) Madalitso Band (Malawi), Mswanu Gogo Vibes (Tanzania), G Clef Taarab Orchestra (Zanzibar) na Afrijam Band (Tanzania).
1.Kutoka kushoto ni Meneja wa Sauti za Busara, Ramadhan Journey, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud, Mwenyekiti wa Bodi wa Tamasha hilo, Simai Said na Balozi wa Norway hapa nchini, Hanne Marie Kaarstad.