
…Wapenzi wenye mgogoro katika mahusiano.
NI Ijumaa nyingine ninapokukaribisha mpenzi msomaji kwenye ukurasa huu, mada yetu ni ile iliyoanza wiki iliyopita. Tulianza kujadiliana kuhusu mada hii kama inavyojieleza.
Nakushukuru msomaji wangu uliyetumia muda wako kunitumia ujumbe mfupi wa maneno au kunipigia na kunieleza ushuhuda wako au kutoa ushauri wa nini cha kufanya inapotokea watu wawili wanaopendana, wakashindwa kupata mtoto.
Nilichokibaini ni kwamba tatizo hili ni kubwa pengine kuliko mtu anavyofikiri, watu wanateseka ndani ya ndoa au uhusiano, hawana pa kusemea wala hawana sehemu ya kupunguzia machungu yao.
Narudia tena kusema, inapotokea mume na mke wameishi kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa kipindi kirefu lakini kukawa hakuna mtoto wala dalili, mwanamke siyo mtu pekee wa kubeba lawama.
Kama ulivyoona mfano wa mama Habiba wiki iliyopita, kwamba alikuwa akituhumiwa kuwa yeye ndiye mwenye tatizo lakini mwisho wa siku alipoachika na kwenda kuolewa na mwanaume mwingine, alipata ujauzito na kujifungua mtoto wa kike.
Jambo la kwanza ambao wanandoa wanaopitia katika kipindi kama hiki kigumu wanatakiwa kufanya, ni kulitambua tatizo linalowasumbua. Lazima wewe na mwenzi wako mkae na siyo mara moja, mara kwa mara, mumwe mnajadiliana kuhusu tatizo linalowasumbua.

Umuhimu wa kuwa mnajadiliana kuhusu tatizo hili ni kwamba nyote mnakuwa kitu kimoja, yaani badala ya kuwa na fikra kwamba mke wangu hazai, kwa kuwa huwa mnajadiliana mara kwa mara, utasema ‘hatupati mtoto’. Yaani mtalichukua tatizo wote wawili na kulibeba na kushirikiana.
Hii ni hatua nzuri sana ya kuanzia kwa sababu utafiti unaonyesha kwamba wanandoa wengi wanaoachana kwa sababu ya kukosa mtoto, huwa ni kwa sababu wao wenyewe hawakuungana na kuliona tatizo kama linawahusu wote wawili na kuamua kulitafutia ufumbuzi.
Mnapokuwa kitu kimoja, ni rahisi kuanza kushughulikia hatua nyingine zinazofuata, kwamba kama ni kwenda hospitali, mtaenda pamoja, kama ni kuhangaikia tiba za asili mtakuwa pamoja pia na watu wanaolishughulikia tatizo hili kwa namna hiyo, hufanikiwa.
Jambo ambalo ningependa kukutoa wasiwasi msomaji wangu, ni kwamba hili tatizo siku hizi linatibika kirahisi kabisa na badala ya kuanza kuhangaika kwa waganga wa kienyeji, wewe na mwenzi wako nendeni hospitali, mkafanyiwe vipimo kisha fuateni ushauri mtakaopewa.
Hatua nyingine ambayo mnapaswa kuifuata mnapokuwa na tatizo kama hili, ni kujiandaa na ‘vita’! Wengi wanaachana siyo kwa sababu hawapendani au wameshindwa kuvumiliana bali ni kwa sababu ya vita wanayopigwa na ndugu, jamaa, marafiki na watu wanaowazunguka.
Mkiwa na tatizo hili, tambueni kwamba mpo vitani, shirikianeni kushinda hila za ndugu wa pande zote, peaneni faraja mnapozungumziwa mabaya, fuataneni machozi na peaneni moyo. Mnapokubali kusikiliza maneno ya nje, mtaacha hata kushughulikia tatizo kwa kwenda kuwaona wataalamu badala yake mtakuwa na kazi ya kulaumiana, kugombana na mwisho kutengana.
Narudia tena, tatizo hili linatibika. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
Hashim Aziz/GPL
Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam