×

Mali ya Bahili Huliwa na Wadudu- 2

SIKUTAKA kuendelea kuwaza zaidi huko kwa kuhofia kujitia wasiwasi na fadhaa. Nilitaka niwaze jinsi ambavyo ningeweza kulimaliza lile tatizo bila kuleta athari kwenye unyumba wangu na mke wangu ambaye licha ya kutopata ujauzito kwa miaka mitatu sasa, nilikuwa bado nampenda.   Asubuhi kulipokucha mimi na mke wangu tukajiandaa kwenda kazini. Nilijua kwa asubuhi ile mke wangu asingeweza kumuuliza kitu hausigeli huyo.    

Mke wangu alikuwa akifanya kazi Shirika la Bandari.  Mimi nilikuwa na kampuni yangu mwenyewe ambayo ofisi yake ilikuwa mitaa ya maktaba.   Asubuhi huwa ninaondoka na mke wangu kwa kutumia gari langu. Humpeleka yeye kazini kwake bandarini kisha ninakwenda ofisini kwangu Barabara ya Maktaba.  

Nilipomfikisha mke wangu kazini kwake, sikwenda ofisini kwangu. Nikarudi nyumbani.  Niliingia ndani na kumfuata Lailatu jikoni.  “Mbona umerudi saa hizi?” Akaniuliza aliponiona nikiingia jikoni.  “Nimerudi kwa ajili yako, mke wangu aliniambia anakushuku kuwa una mimba, je ni kweli una mimba?”  

SASA ENDELEA.  

LAILATU aliinamisha kichwa chini kabla ya kunijubu.   “Naona ninayo.”  Moyo ukanilipuka.  “Ni ya miezi mingapi?”  “Itakuwa miwili.”  “Sasa kwanini hujaniambia?”  Lailatu hakunijibu.  “Hiyo mimba ni ya nani?”  “Ni ya kwako.”  “Sasa kwanini hujaniambia mpaka mke wangu amekugundua kuwa una mimba. Huoni kwamba utaniletea matatizo?”

“Niliogopa kukwambia.”   “Kwa hiyo ulitaka mke wangu agundue.”   Lailatu akatikisa kichwa bila kujibu kitu.  “Sasa tutaliepusha vipi hili tatizo?” “Mimi nakusikiliza wewe.”  Nilinyamza kwa sekunde tano hivi kufikiria kisha nikamwambia.

“Sikiliza nikwambie, nitakupa nauli pamoja na pesa kidogo urudi kwenu Korogwe. Mke wangu akirudi mchana mwambie umepigiwa simu, mama yako anaumwa na ana hali mbaya sana hivyo unahitajika uondoke kesho asubuhi kwenda Korogwe.

Umenielewa?”  “Sawa.”   “Nimeona ukiendelea kukaa hapa, mke wangu akithibitisha kuwa una mimba kweli atataka kujua amekupa nani wakati  wewe unashinda humu humu ndani…”   Lailatu alikuwa amenyamaza kimya akinisikiliza.

Nikatia mkono mfukoni mwangu na kutoa shilingi elfu themanini na kumpa.  “Utafanya nauli na nyingine utatumia ukiwa huko Korogwe.  Ukimwambia mama yako kuhusu hiyo safari kesho atakupa  mshahara wako. Sawa?”  Lailatu akanitazama  mara moja kama aliyetaka kuniuliza kitu lakini alishindwa kuuliza akaurudisha uso wake chini.

Pengine alitaka kuniuliza nani atailea ile mimba. Au alitaka kuniuliza kama nitakuwa na mawasiliano naye akiwa huko Korogwe lakini kwa sababu ya aibu alishindwa kuniuliza.   “Sasa mimi  naenda kazini, usisahau hivyo nilivyokwambia,”nikamwambia.  “Akija tu nitamwambia.”

“Mwambie kesho unahitajika  uende Korogwe…” nikamsisitizia.  “Sawa. Nitamwambia.”   “Kama atakuuliza tena kuhusu mimba mwambie huna mimba. Usimkubalie kabisa. Ukiondoka chukua nguo zako zote.”  “Sawa.”   Nikaondoka na kwenda kazini kwangu huku moyo wangu ukiwa umetulia kidogo.   Nikiwa ofisini  kwangu nilijiuliza kama yule msichana ataweza kumueleza mke wangu kama nilivyomfundisha.

Nilijiambia kama atashindwa kumueleza sawa sawa, mke wangu ni mjanja anaweza kugundua kitu.  Anaweza kugundua kuwa yule msichana anadanganya na kuna kitu anakificha.  Baya zaidi, niliendelea kujiambia, ni endapo atagundua kuwa  Lailatu anataka kuondoka ili kuficha ile mimba  yake isijulikane. Atakapogundua hilo atajiuliza kwa nini Lailatu anaficha mimba yake?

Ni nani aliyempa mimba ile wakati hana uhusiano na mwanaume yeyote wa nje? Anaweza akaanza kunishuku mimi.  Jioni niliporudi nyumbani nilimkuta mke wangu chumbani akipanga nguo zilizofuliwa.  “Habari za hapa?” nikamuuliza.  “Nzuri, za kazi.”  “Nashukuru ni nzuri.”  Alinisubiri nivue koti langu kisha akaniuliza.   “Huyu Lailatu hujampa pesa?”

  Moyo ulinilipuka kama niliyepigwa na shoti ya umeme!  Hapo hapo nikajiona nimeanza kupumua kwa nguvu kama ambaye nilikuwa nakimbia.   “Kwani ni umeniuliza hivyo?”  “Nijibu kwanza halafu nitakwambia.”   Nikajiuliza Lailatu amemwambia mke wangu kuwa nimempa pesa ili  arudi Korogwe kuficha ile mimba ambayo nimempa mimi?   Sikupata jibu. Nikajaribu kuondoa ile hofu kisha nikamwambia mke wangu.  “Sijampa pesa.”   Nilikuwa nimeshaamua kumkana japokuwa ilikuwa kweli nimempa pesa hizo.

“Niliporudi kutoka kazini ameniambia kuwa amepigiwa simu na mjomba wake kuwa mama yake ni mgonjwa huko Korogwe, yaani anatakiwa aende kesho asubuhi. Lakini nikagundua kuwa alikuwa na pesa amezifunga kwenye nguo karibu shilingi elfu themanini.” Mke wangu akaniambia na kuendelea.  “Nikamuuliza hizo pesa amezipata wapi, akaniambia ametumiwa na kaka yake aliyeko Arusha kwa ajili ya matibabu ya mama yake…”

Nilikuwa nikiyasilikiliza kwa makini yake maneno.   “Mimi hata sikuamini.” Mke wangu aliendelea kunieleza. “Nikamwambia anioneshe hiyo meseji iliyotuma hizo pesa, akaniambia ameshaifuta lakini nilipotazama ile simu yake nikaona  namba ambazo sikutegemea kuzikuta katika simu yake”  “Ulikuta namba gani?” nikamuuliza.

“Nilikuta namba yako wewe katika sehemu inayoonesha simu alizopokea. Simu yake inahifadhi namba. Akipiga au akipigiwa namba inabaki.”  Nikashituka tena kwani ni kweli nilishawahi kumppigia simu.  “Uliona nimempigia leo?”  “Si leo. Nimeona kwenye namba za tarehe ya nyuma. Ngoja nimwambie anipe simu yake nikuoneshe.”

“Haina haja. Kama ni tarehe za nyuma nilishawahi kumpigia lakini sikumbuki nilimpigia kumueleza nini. Kwani kuna tatizo gani?”  “Tatizo ni hilo. Nilipomuona na zile pesa na nilipoona namba yako kwenye simu yake nikashituka na kudhani labda ni wewe uliyempa.”   “Nimpe pesa hizo za nini? Kwani si alikwambia pesa hizo alitumiwa na kaka yake kwa ajili ya matibabu ya mama yake?”

ITAENDELEA