Mtunzi: Kulwa Mwaibale
Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale mama Careen na Cathe alipokuwa mezani akila na mabinti zake hao, kila mmoja akawa anatafakari ishu ya mapenzi ndipo mama huyo akajikuta akitabasamu kufuatia kitendo cha kutoka na mabwana wawili kwa muda mfupi. Careen alipomwuliza kilichomfurahisha akawaambia kuna jambo f ’lani, Cathe akamwuliza labda alipata fedha, akamwuliza alijuaje?
Je, nini kilifuatia? Songa mbele sasa…
MAMA huyo alipomwuliza alijuaje kama alipata fedha, Cathe ambaye siyo muongeaji sana alicheka na kusema:
“Jamani mama, si akina baba wamekuja?”
“Kumbe na wewe siku hizi umekuwa muongeaji namna hiyo, kweli huko chuoni wamekuchangamsha,” mama yao alimwambia Cathe, wote wakacheka.
“Hujakosea, kuna mambo mawili yaliyonifurahisha, kubwa nimepata hela lakini lingine ni siri yangu,” mama huyo aliwaambia wanawe.
Alipotoa kauli hiyo, kabla Careen aliyetaka kushadadia jambo hajasema chochote, simu ya mama yao ikaanza kuita, wakatulia kupisha mama yao azungumze na aliyempigia.
Mpigaji wa simu hiyo alikuwa pedeshee Jacks aliyemwuliza mama Careen alishindaje na uchovu aliomuacha nao baada ya kumgaragaza fasta, akamwambia alishinda vizuri.
Ili kujiachia zaidi kimazungumzo na Jacks, mama huyo ambaye muda huo alivaa kaptura ya kitenge iliyomkaa vizuri na kuyaonesha vyema makalio na mapaja yake na kisingleti cheupe, aliinuka na kuelekea chumbani kwake.
“Umeiona shepu ya mama yako? Halafu huyo sijui ni baba mwingine au ni kati ya wale waliokuja!” Careen alimwambia pacha wake.
“Mama siyo mchezo, Mungu amemjalia shepu ya ukweli
kama watu wanavyotuambiaga sisi, mwenzangu hata mimi nashindwa kutabiri kama ni mmoja wa akina baba waliokuja au mwingine,” Cathe alimwambia mwenzake, wakacheka.
“Tuachane naye, kama atapenda kutuambia ni nani, atafanya hivyo akirudi, tuendelea kumanga msosi,” Careen alimwambia pacha wake.
Kule chumbani mama yao aliongea kwa muda na Jacks aliyeamua kuwapa chakula cha usiku siku hiyo ambapo mama huyo aliifurahia sana ofa hiyo hasa ukizingatia tangu mabinti zake waliporejea kutoka chuoni alikuwa hajatoka nao out.
Alipomaliza kuzungumza na Jacks, akiwa na furaha alirudi sehemu ya kulia chakula na kuwaambia mabinti zake baadaye wajiandae kwa mtoko, chautundu Careen aliposikia hivyo alisimama na kushangilia.
“Hiyo ndiyo habari njema mama, hapo mama umefunika tena kwa funiko la chuma, zege cha mtoto!” Careen alimwambia mama yake, wote wakacheka.
“Ndiyo hivyo, atakayependa kuvunja kabati avunje, atakayependa kuvaa kama anakwenda kanisani avae, ofa ndiyo hiyooo imejileta,” mama huyo aliwaambia wanawe, wakacheka.
Walipomaliza kula, mapacha hao waliofurahi kutolewa out, waliosha vyombo na kufanya usafi jikoni, walipomaliza mama yao aliwaita sebuleni.
“Hebu tuzungumze kidogo wanangu, naona huu ndiyo muda muafaka,” mama huyo aliwaambia wanawe hao.
Mabinti zake, wakiwa wametulia kusubiri watakachoambiwa, mama yao aliwafahamisha kwamba ofa ya kutoka out jioni hiyo ilitolewa na Jacks aliyemtambulisha kwao mapema.
Akawafahamisha kwamba Jacks alikuwa msaada mkubwa sana katika maisha yao na kwamba ada yao ya mwaka wa mwisho na matumizi yao yote aliyatoa yeye hivyo wamheshimu kama baba yao.
Mama huyo aliongeza kuwa, Jacks anaweza kufika pale nyumbani muda wowote na kupumzika na wakiwa na tatizo wamwambie bila shaka, akina Careen wakamshukuru mama yao.
Alipomaliza kuwaeleza habari za Jacks akawaambia kulikuwa na jamaa mwingine anaitwa Michael a.k.a Meco ambaye aliyebahatika kumuona alikuwa Careen aliyemkaribisha ndani.
“Meco naye wanangu amekuwa msaada mkubwa sana
katika maisha yetu, saluni ninayomiliki alinifungulia na gari ninalotembelea ameninunulia yeye, kule Kinyerezi kaninunulia uwanja na tayari ujenzi umeanza,” mama huyo aliwaambia mabinti zake.
“Hongera mama yetu, una bahati ya kupendwa na akina baba wenye fedha zao,” Careen alimwambia mama yake.
Mama huyo alipopewa hongera alifurahi sana bila kujua tabia yake ya kuwachanganya wanaume ingewaharibu wanawe, akasema:
“Meco naye yupo huru kufika hapa nyumbani kama ilivyo kwa Jacks.”
Alipotoa kauli hiyo, Careen na Cathe waliduaa kwani japo hawakuanza mambo ya mapenzi walijua hatari ambayo mama yao aliitengeneza, Careen akamwuliza:
“Hivi mama hao akina baba wanafahamiana?”
Badala ya kuonesha mshtuko, mama yao alicheka na kuwaambia hawakufahamina na wasingefahamiana kwani alikuwa anajua namna ya kuishi kwa akili na wanaume wenye fedha waliokuwa wakiwasaidia.
Kufuatia kauli hiyo ya mama yao, Careen na mwenzake wakawa wapole, utafikiri waliambiana kila mmoja moyoni mwake akasema watajadili jambo hilo watakapokuwa peke yao.
Mama huyo akaendelea kuwaambia kwamba, katika maisha alichoangalia ni kupata fedha na kwamba hakuwa na habari na wanaume wachovu ndiyo maana aliweza kuwalea na kuwasomesha hadi chuo kikuu bila matatizo.
Baada ya kuzungumza na mapacha wake hao, alikwenda kwenye kabati la runinga akafunua kitambaa na kutoa shilingi laki tatu, akawapatia wanawe hao wa pekee na kuwaambia kesho yake waende mjini wakafanye shopping.
Kama ilivyokuwa kawaida yake, Careen chautundu akiwa kazishika zile fedha, aliinuka na kushangilia akisema:
“Ndiyo maana tunakupenda sana mama yetu wa ukweli, Mungu akuzidishie maisha marefu uje uwaone mpaka wajukuu zetu.”
Alipotoa kauli hiyo, wote walicheka ndipo mapacha hao walimshukuru mama yao aliyewaambia wasijali atahakikisha hawakwami kwa chochote hata siku moja bila kujua Jacks aliyempa ofa na mabinti zake, alikuwa na lake jambo.
Je, ni jambo gani hilo? Usikose uhondo huu wiki ijayo. Kwa maoni, tuma kwenye namba hiyo hapo juu.