×

Insane (Mwendawazimu)-11

ILIPOISHIA

“Ni nani anamfanya huyu msichana kunichunia hata nikimsalimi? Au hajui kama mimi ni mtoto wa bilionea? Subiri! Nitamfuata tu na si kuishia kumsalimia,” alijisemea, wakati akizungumza hayo, miguu aliweka juu ya meza ambapo hapo kulikuwa na mabunda ya hela aliyokuwa ameyapanga. Kwa hesabu za harakaharaka zilikuwa kama milioni kumi na tano.

Wanafunzi wote wakawa wakimtolea macho, ila yeye hakujali.

SONGA NAYO

 

Fabian alikuwa na kukua. Uwezo wake darasani ulikuwa mkubwa na haukupungua. Hakuwa mtu wa kushika nafasi ya pili, kila mtihani ulipokuwa ukifanyika, alitoka nafasi ya kwanza.

Boniface alifurahi kuwa na mtoto kama Fabian ambaye kila siku shauku yake ilikuwa ni kusoma kwa bidii kubwa. Mpaka anamaliza kidato cha nne, Boniface hakutaka kumuoa Jesca, alikuwa akiishi naye na alijiahidi kwamba asingeweza kumuoa msichana yeyote kwa kuogoipa kumuumiza Miriam.

Hakuacha kwenda Dodoma kumuona mama watoto wake, kila alipokwenda huko, alikaa sehemu na kuzungumza naye. Hakuwa akieleweka lakini katika maisha yake alikuwa mtu muhimu kuliko mtu yeyote katika maisha yake.

“Kuna siku utapona Miriam, halafu nitakuoa. Hata kama tutakuwa wazee, nitakuoa hivyohivyo,” alisema Boniface huku akimwangalia mwanamke huyo mwendawazimu.

Baada ya kumaliza kidato cha sita na kufanya vizuri, Fabian akafanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alifurahi kwa sababu maishani mwake, kujiunga na chuo hicho ilikuwa moja ya ndoto zake za kuwa daktari hapo baadaye.

Siku ya kwanza kuingia darasani, akakaa kwenye kiti, akainamisha kichwa chake na kuanza kusali. Alimshukuru Mungu kwa safari yake ndefu, na hapo alikuwa akimuomba kwa ajili ya safari yake nyingine aliyotaka kuianza.

Wakati akiwa amekiinamisha kichwa chake, ghafla akajikuta akishikwa na mwanachuo mmoja, akakiinua kichwa chake, macho yake yakagongana na macho ya msichana mmoja mrembo aliyekuwa akimtolea tabasamu pana.

“Naitwa Esther Innocent…” alisema msichana huyo huku akiwa na tabasamu pana.

“Naitwa Fabian Boniface. Nikusaidie nini Esther?” aliuliza Fabian huku akitetemeka, hakuwahi kuzungumza na msichana ambaye alihisi moyo wake ukianza kumpenda.

“Nimekuja kukusalimia. Naomba uwe mwenyeji wangu…” alisema Esther.

“Mimi mwenyewe mgeni. Ungemtafuta mwenyeji…” alidakika Fabian harakaharaka.

“Sawa. Basi naomba kampani yako!”
“Ya nini?”
“Urafiki tu. Tuwe tunasoma wote.”

“Hakuna tatizo. Ila unaonekana kama unanifahamu!”

“Ndiyo!”
“Ulishawahi kuniona wapi?”

“Tambaza!”
“Mmh!”

“Ndiyo! Ila usijali! Ninahitaji kampani yako Fabian.”
“Basi haina shida. Ila kuna sharti moja. Sipendi mambo ya mapenzi!”

“Hilo wala siyo tatizo. Nitatii sharti lako,” alisema msichana huyo huku akiachia tabasamu. Japokuwa aliweka sharti lake lakini moyoni mwake alihisi kwamba asingeweza yeye mwenyewe asingeweza kuvumilia. Hakuona kama ingewezekana kuweka urafiki na msichana mrembo kama alivyokuwa Esther. Moyoni mwake, akahisi kabisa kwamba yeye ndiye angekuwa mtu wa kwanza kulivunja sharti hilo.

****

Alikuwa miongoni mwa wasichana warembo katika Shule ya Sekondari ya Kisutu jijini Dar es Salaam. Hakuwa mzungumzaji sana, alikuwa mkimya na mpole kiasi kwamba wasichana wenzake katika shule hiyo walimpa jina la Mama Theresa ingawa jina lake halisi lilikuwa Esther Emmanuel.

Alikuwa na sura nzuri, alipendeza kwa kila nguo aliyovaa, shuleni, alikuwa na uwezo mkubwa, alipendwa kutokana na upole wake na kila alipokuwa, wanafunzi wenzake walimzunguka huku kila mmoja akitaka kusikia chochote kutoka kwake, hasa kuhusiana na masomo.

Hakupenda wanaume, alikuwa akiishi kivyake, nyumbani kwao, baba yake alikuwa mchungaji wa kanisa la Kilokole la Praise And Worship. Muda mwingi alipokuwa akikaa darasani, alikuwa akiimba nyimbo za Injili kutoka katika kitabu kidogo cha Tenzi za Rohoni.

Hakupenda mapenzi, hakupenda kuwa na mwanaume yeyote katika maisha yake mpaka pale atakapoolewa. Wanaume wengi walimfuatilia, hasa nyumbani kwao, Sinza Kijiweni lakini hakukuwa na aliyempata, hakuwa akionekana nyumbani, muda mwingi alikuwa akijifungia na alipokuwa akionekana, alikuwa akienda shuleni au kanisani.

Alipokuwa akiimba, sauti yake nzuri ilimvutia kila mwanaume, aliimba kwa sauti kali kiasi kwamba kanisa lao likawa likimtumia mara kwa mara kuwa kiongozi wa waimbaji katika mikutano mbalimbali ya Injili.

Kila mtu alimheshimu, pamoja na kupewa jina la Mama Theresa kutokana na upole wake lakini wakati mwingine watu walikuwa wakimuita sista kwa kuamini kwamba mpaka kipindi hicho hakuwa amekutana kimwili na mwanaume yeyote yule.

Baada ya kukaa kwa kipindi kirefu shuleni pasipo kuwa na mwanaume yeyote ndipo akaanza kupata taarifa kwamba kulikuwa na mwanaume aliyekuwa na akili sana, mwanaume ambaye alikuwa gumzo katika shule nyingi za sekondari, mwanaume huyu alijulikana kwa jina la Fabian Boniface.

Akatokea kumpenda hata kabla hajamuona, mara kwa mara akawa anamfikiria na siku ambayo alikutana naye ilikuwa siku ya kongamano kubwa lililofanyika katika Viwanja vya Jangwani.

Hapo ndipo alipomuona baada ya kuoneshwa. Moyo wake ukaendelea kumpenda, alikuwa mwanaume mwenye sura nzuri, mpole ambaye aliona kabisa kama angekuwa naye basi angeweza kumfanya kuwa na furaha maishani mwake.

“Ila nimeokoka!” alijisemea.

Moyo wake ukachukuliwa na kutawaliwa na mwanaume huyo, alimpenda, wakati mwingine alijua fika kwamba alifanya kosa kumpenda mvulana huyo kwa kuwa aliokoka lakini hakuwa na jinsi.

Akatamani kumtoa moyoni mwake, akashindwa, akatamani kutokumfikiria, akashindwa, akatamani kutolitaja jina lake kwa siku, napo akashindwa. Akili yake ikachanganyikiwa, alitamani sana kumwambia ukweli kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake lakini ikashindikana.

Baada ya miaka miwili, akakutana na mvulana huyo chuoni. Alijua kwamba kulikuwa na wanawake warembo ambao wangeweza kumpiku, alichokifanya, harakaharaka kumfuata na kuanza kuzungumza naye kwani bila hivyo, kungekuwa na mwanamke mwingine ambaye angemchukua mwanaume huyo.

“Nitahitaji kuwa na wewe zaidi,” alisema Esther.

“Kivipi?”
“Urafiki tu! Kwani kuna ubaya?”

“Hapana! Ila sihitaji mpenzi kwa sasa…”

“Hata mimi sihitaji mpenzi. Ninahitaji rafiki kwanza,” alisema Esther.

Alikuwa akizungumza na Fabian, moyo wake ulimpenda mno, kila alipomwangalia, aliona mapenzi mazito yakiwa yameufunika moyo wake. Hakutaka kumkosa, alitamani kuendelea kuwa rafiki yake kwani mbele yake aliona ndoto kubwa wakiishi pamoja na kutengeneza familia pamoja.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa urafiki wao, wakawa pamoja. Kila mtu aliyewaangalia watu hao, aliona kabisa kwamba walikuwa wapenzi kwani kila kona waliyokuwepo, walikuwa wawiliwawili tu.

Wakaanza kuwa gumzo kwa wanafunzi waliokuwa wakisomea utabibu chuoni hapo. Hawakujali, hawakuwasikiliza watu walisemaje, walichokuwa wakikijua ni kwamba walikuwa marafiki wa kawaida japokuwa kila mmoja alianza kumpenda mwenzake.

“Hizi tetesi zinanikera sana,” alisema Fabian, aliyazungumza hayo huku akimwangalia Esther machoni, alitaka kujua angejisikiaje.

“Zipi hizo?”
“Hizi za mimi na wewe kuwa wapenzi! Hivi unazionaje?” aliuliza.

“Mbona kawaida.”
“Hapana! Sizipendi kwa sababu sisi siyo wapenzi, ni marafiki tu,” alisema Fabian.

Moyo wa Esther ukanyong’onyea, moyoni mwake ukahisi maumivu makali, akaona kama kulikuwa na mtu alimfuata na kisu kisha kuuchoma moyo wake. Alimwangalia vizuri Fabian na kujiuliza kama kile alichokizungumza alimaanisha au la. Uso wake tu, ulionyesha ni jinsi gani alimaanisha.

Alitamani kumwambia Fabian ukweli kwamba alikuwa akimpenda lakini alishindwa kujua ni wapi alitakiwa kuanzia, wakati mwingine alitamani hata kumtuma mtu ili amwambie lakini alishindwa kufanya hivyo.

Moyoni mwake aliona aibu kubwa, alikuwa mlokole, mtoto wa mchungaji, muimba kwaya, tena kanisani alikuwa akisimama mstari wa mbele kabisa, angefanya nini na angeanzia wapi kumwambia Fabian kwamba alikuwa akimpenda?
Hakuwa na jinsi, aliamua kunyamaza lakini wakati mwingine alijiona kama akichelewa kwani kama asingemwambia ukweli, kulikuwa na msichana ambaye angekuja na kumwambia ukweli.

Kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwa mwanaume huyo, wivu ukaanza kumkamata kila alipomuona Fabian akizungumza na wasichana wengine. Alitamani kumwambia namna alivyokuwa akijisikia moyoni mwake lakini akashindwa kabisa.

“Ninakupenda Fabian…ninakupenda mpenzi!” alijisemea huku akijiangalia kwenye kioo.

Wakati yeye akiwaza hilo, hata kwa Fabian ilikuwa hivyohivyo. Alimpenda Esther lakini hakujua alitakiwa kuanzia wapi. Moyo wake uliteseka, usiku hakuwa akilala vizuri kwa sababu ya mawazo.

Alihisi tu kwamba Esther alikuwa akimpenda lakini hakuwa na uhakika juu ya hilo. Alimchukulia kama rafiki yake, kitendo cha msichana huyo kuwa mtu wa dini sana, kuimba sana nyimbo za dini na kusoma sana Biblia ikamuogopesha na kuona kama angemwambia kuhusu mapenzi basi angemkaripia.

“Kweli nimwambie? Nianzaje sasa? Mhh!” alijiuliza pasipo kuwa na majibu yoyote yale.

Wakati akijiuliza sana, akasikia simu yake ikianza kuita, harakaharaka akaichukua na kuanza kuangalia kioo cha simu ile. Namba ilikuwa ngeni, hakujali sana kwani alikuwa akipigiwa sana simu na namba za aina hiyo, alichokifanya ni kuipeleka sikioni.

“Nisikilize wewe kijana. Nimesikia unatembea na msichana wangu! Nimesikia unajibebisha tu kwa demu wangu. Sasa nakwambia kitu kimoja, achana naye, kama unataka kuwa salama maishani mwako bora uachane naye kwani vinginevyo nitakuteka na kukuua,” ilisikika sauti ya mwanaume kwenye simu hata kabla ya salamu.

“Natembea na msichana wako?” aliuliza Fabian huku akishtuka.
“Ndiyo! Nasikia unatembea na Esther. Nimesikia taarifa hizo na nimewatuma watu wafuatilie na kweli imegundulika kwamba upo naye, tena kwa kumganda kama ruba. Sasa ninakupa nafasi ya kwanza na ya mwisho kuachana naye. Vinginevyo, utajikuta porini ukiwa umezungukwa na mabaharia…” alisikika mwanaume huyo kwenye simu.

“Unasemaje?”

“Tip tip tip…” simu ililia kuonyesha kwamba ilikatwa.

Fabian hakujua ni nani alimpigia simu na hakuelewa alikuwa akimzungumzia msichana yupi. Alichanganyikiwa, aliiangalia simu yake kana kwamba aliambiwa kuwa mtu huyo angempigia simu tena.

Alichokifanya, akaipiga simu ile lakini haikuwa ikipatikana. Moyo wake ulimuuma mno kwani alikuwa akihitaji kumfahamu mtu huyo na kile alichokuwa akikizungumzia. Akaelekea kitandani na kutulia huku akionekana kuwa na mawazo.

Hakukuwa na msichana ambaye alikuwa karibu yake kwa kipindi hicho zaidi ya Esther, ndiye ambaye alishinda naye na hata kula naye, na darasani walikuwa pamoja hivyo akajua huyo mwanaume aliyempigia simu alikuwa mpenzi wa Esther tu.

Hilo likamuweka kwenye wakati mgumu, akabaki akiwa na mawazo tele na muda mwingi alikuwa akifikiria ni kitu gani alichotakiwa kufanya kwani kumuacha Esther hakupenda lakini pia maneno aliyoambiwa, hakika yalimtisha.

“Itakuwaje? Nimuache Esther kweli? Ila naweza kutekwa, huyu mtu inaonekana hatanii hata kidogo,” alisema Fabian huku akionekana kuchanganyikiwa.

Uamuzi aliofikia ulikuwa ni kumuacha Esther, hakutaka kuwasiliana na msichana huyo na kuanzia hapo, kila alipokuwa akipigiwa simu, hakutaka kupokea kwani aliogopa kuendeleza ukaribu na msichana huyo.

“Sitaki Esther, naomba uniache,” alisema Fabian huku akiiangalia simu yake.

Esther hakuchoka, hiyo haikuwa kawaida kutokea, mara kwa mara alikuwa akimpigia simu Fabian lakini haikuwa ikipokelewa. Jambo hilo lilimuumiza kichwa sana, akawa na mawazo, alichanganyikiwa kwa penzi la mwanaume huyo na kile kilichokuwa kikitokea hakika kilimchanganya.

Siku iliyofuata, Esther alipofika chuo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtafuta Fabian, alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Haikuwa kazi kumpata mwanaume huyo, alipompata, akataka kuzungumza naye.

Siku hiyo Fabian alionekana kuwa tofauti sana, alishangaa, jana alimuacha akiwa na furaha tele lakini ghafla akabadilika, hakuonekana kuwa na furaha tena, ule uso wa tabasamu ambao alizoea kuuona kwa mwanaume huyo, hakuuona tena kitu kilichouumiza moyo wake.

“Kuna nini?” aliuliza Esther huku akionekana kutokuelewa chochote kile.

“Hakuna kitu!”
“Umebadilika, tatizo nini mpenzi?” aliuliza Esther.

“Naomba uniache Esther!”

“Nikuache? Tatizo nini mpenzi? Naomba uniambie,” alisema Esther.

Fabian akanyamaza, hakutaka kumwambia kile kilichokuwa kimetokea kwani kwa jinsi alivyowajua wanawake, ilikuwa ni lazima kukataa na kujifanya hamfahamu mwanaume huyo.

Moyo wake uliamua kwamba hakutaka kuwa na msichana huyo, vitisho alivyopewa na mwanaume ambaye hakuwa akimfahamu vilimuogopesha kupita kawaida. Alimwangalia msichana huyo, ni kweli alimpenda lakini hakuwa radhi kujiona akiuawa kwa sababu ya mapenzi, aliyapenda maisha yake mno.

“Esther! Naomba uniache…” alisema Fabian kwa msisitizo.

“Kwa hiyo umeamua kukataa kuniambia tatizo nini?” aliuliza Esther.

“Naomba uniache!”

“Naomba nikuulize kitu Fabby! Unanipenda?” aliuliza msichana huyo.

“Ninakupenda…”
“Tatizo nini?”
“Nahitaji uniache tu! Hakuna kingine!” alisema Fabian.

Moyo wake uliumia, hakuamini kama kweli yeye ndiye alikuwa na ujasiei wa kumwambia Esther maneno kama yale. Moyo wake ukajigawa, upande mmoja ulimwambia kwa kile alichokifanya kilikuwa vizuri kwa kuwa alikiepuka kifo lakini upande mwingine ulikuwa ukimlaumu kwa sababu uzuri wa Esther hakutakiwa kuachwa na mwanaume yeyote yule.

Hakutaka kusimama mbele ya msichana huyo, alichokifanya ni kuondoka. Esther akabaki akimwangalia Fabian, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea. Alihisi kwamba kulikuwa na kitu kimetokea kwani halikuwa jambo la kawaida kwa mwanaume kuamua hivyo ghafla, kama alikuwa na mpango wa kumuacha kisa amepata msichana mwingine, angefanya hivyo kwa taratibu na si kwa haraka kama alivyofanya.

Pale aliposimama, alihisi miguu yake ikitetemeka, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia hatua hiyo. Akajaribu kumuita Fabian, sauti haikutoka kwani tayari alianza kulia kilio kilichojaa kwikwi huku machozi yakimtoka na kutiririka mashavuni mwake.

Wakati hayo yote yakiendelea, Theo alikuwa akifuatilia kila kitu. Moyo wake ukafarijika kwani hakukuwa na kitu alichotamani kitokee kama kumuona Fabian akiachana na Esther huyo ili yeye apate nafasi ya kuwa na msichana huyo mrembo.

Hiyo ikaonekana kuwa nafasi yake, hakutaka kufanya harakaharaka, alichokifanya ni kutulia mpaka pale ambapo angeona kuwa muda sahihi wa kumfuata na kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda.

Baada ya siku mbili za majonzi tele kwa Esther, Theo akaanza ukaribu na msichana huyo, ilikuwa ngumu kwake kumzoea kwani muda mwingi alionekana kuwa na mawazo tele, mapenzi bado yaliutesa moyo wake.

“Esther…” aliita Theo. Msichana huyo hakuitia, akageuza macho na kumwangalia Theo.

“Naona una huzuni sana, tatizo nini?” aliuliza Theo huku akimwangalia msichana huyo machoni, naye akajifanya kuwa na huzuni.

“Naomba uniache wewe kaka,” alisema Esther.

“Samahani! Nimekuja kukujulia hali, unaonekana mnyonge sana, sidhani kama nimefanya kosa, sidhani kama ni kosa kumjulia hali mgonjwa, tatizo nini?” aliuliza Theo.

“Naomba uondoke…”

“Daah!”

Esther akasimama na kuondoka zake huku akimuacha Theo mahali hapo. Hilo wala halikuwa tatizo, aliamini kwamba mara zote unapomfuatilia msichana, unaanza kwa ugumu lakini mwisho wa siku kila kitu kinakuwa kama unavyotaka.

Hakuacha, aliendelea kumfuatilia msichana huyo zaidi. Kila siku ilikuwa ni lazima kuzungumza naye huku akimtaka kujua tatizo lilikuwa nini. Kwa Esther, kikafika kipindi akachoka, hakutaka kuona mwanaume huyo akija kwake na kumnyamazia kama alivyokuwa akifanya.

Alichokifanya ni kuanza kuzungumza naye. Kwa Theo, hicho ndicho alichokuwa akikihitaji. Akamuonyeshea uchangamfu mkubwa ambao Esther hakuwahi kuuona sehemu yoyote ile, alimshangaa sana Theo kwani kwa jinsi alivyokuwa mcheshi, ilikuwa ngumu sana kumchoka.

Ukawa mwanzo, wakaanza hivyo. Theo hakutaka kuacha, alichoamua kilikuwa ni kumpoteza kabisa Fabian moyoni mwa msichana huyo. Hiyo, haikuwa kazi nyepesi kwani wakati mwingine alimfurahisha Esther lakini alipopita Fabian, msichana huyo alinyamaza na kumwangalia mwanaume huyo, alitamani kumuongelesha lakini aliamua kunyamaza tu.

“Kuna nini?” aliuliza Theo huku akijua kabisa kilichokuwa kikiendelea.

“Naomba tuondoke hapa!”
“Kwa nini?”
“Nataka kuwa na furaha! Naomba tuondoke hapa,” alisema msichana huyo. Theo hakuwa na jinsi, akakubaliana naye na kuondoka mahali hapo.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.