×

Ahukumiwa Mahakamani kwa Kumtisha Mwanamke Anayempenda

MUTARE, Zimbabwe

Inaweza ikakushangaza lakini ndiyo ukweli wenyewe uliotokea nchini Zimbabwe ambapo jamaa aitwaye Allan Zarema amejikuta akikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kumsumbua Pinkie Makurumidze kwa kumwambia anampenda kila siku.

Pinkie ameieleza mahakama kwamba Allan amekuwa akimsumbua kila siku kumwambia kwamba anampenda na wakati moyo wake haupo kabisa kwa mwanaume huyo na kuona kwamba ni usumbufu ambapo aliamua kumfikisha mahakamani kitu kilichowashangaza watu wengi.

“Amekuwa akinifuata kila siku, tena wakati mwingine usiku wa manane na kuniambia kwamba ananipenda, amenifanya kukosa amani kila siku,” Pinkie aliieleza mahakama na kuongeza:

“Mara nyingine amekuwa akija nyumbani kwangu, anarusha mawe dirishani na kusema kwamba endapo nitamkataa, basi atanifanyia kitu kibaya,” alisema Pinkie.

Japokuwa Allan aliitwa mahakamani na mahakama lakini hakutaka kwenda hivyo hakimu wa Mutare aitwaye Nyasa Kuture kumhukumu kwa kumzuia kwenda nyumbani kwa Pinkie kwa muda wa mwaka mzima.

Hilo si tukio la kwanza la aina yake kutokea nchini Zimbabwe kwani mwaka 2014 katika Mji wa Kadoma, polisi alipigwa vibaya baada ya kumkamata kijana wa miaka 20 kwa kosa la kumsumbua mke wa mtu.

Na Nyemo Chilongani/GPL