The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-04

Sarafina hakuwa na habari na Richard, kwake, mwanaume huyo alionekana kuwa mtu wa kawaida, asiyejiweza ambaye hakuwa na uhakika kama angeweza kumnunulia hata wigi la Kibrazil. Hakutaka kuwa naye, umasikini wa nyumbani kwao ulikitesa kichwa chake na hakukuwa na kitu kingine alichokifikiria kama kupata pesa za kuweza kufanya kila kitu.

Alihitaji nguo, vipodozi na vitu vingine vingi kwa ajili ya maisha yake hivyo hakuona kama kulikuwa na sababu ya kuwa na mwanaume ambaye hakuwa na pesa.

Aliendelea kutanua, david hakuwa na hiyana, alimpa Sarafina kila kitu alichokuwa akikihitaji lakini pia naye alipata kila kitu alichokuwa akikihitaji kwa msichana huyo. Mapenzi yakamchanganya Sarafina, hakumfikiri mwanaume yeyote yule, kwake, David alikuwa zaidi ya mtu yeyote yule, kwake, hakukuwa na mwanaume ambaye alikuwa na thamani kubwa kama David.

Chuoni wakajua, watu wengi wakashangaa, sarafina hakutakiwa kuwa na mtu kama David, mwanaume huyo alikuwa mtu wa wanawake, aliwafunua wanawake wengi chuoni hapo, aliwafanya alivyotaka, wanawake wengi walilia kwa ajili yake, wengi walitoa mimba kwa kuwa alikuwa akizikataa, kitendo cha Sarafina kuwa na mwanaume huyo ilionekana kuwa kama marudio ya maisha ya wasichana wengine kwamba naye angepatwa na balaa kama yaliyowapata wanawake wengine.

“Sarafina! Ninakupenda, ninakupenda sana,” alisema David huku akimwangalia msichana huyo machoni.

“Nakupenda pia!”

“Ungependa twende wapi?”
“Maisha Basement! Nimesikia kuna wasanii, Diamond na Ali Kiba watapanda jukwaani kwa pamoja kutambulisha ngoma yao mpya. Jamani! Nawapenda wale mpaka naumwa!” alisema Sarafina huku akimwangalia David.

“Hakuna shida!”

Maisha ya starehe yakamteka msichana huyo, alikwenda huku na kule akila raha, kwake, kila kitu kilionekana kuwa chepesi kwa kuwa tu alikutana na mwanaume aliyekuwa tayari kumpa kiasi kingi cha fedha kwa ajili ya kufanyia mambo yake.

Hakutaka kumfikiria Richard, kila alipokuwa akimuona chuoni hapo, alimuonea huruma, alionekana kuwa mwanaume mwenye maisha duni, mwanaume ambaye alitakiwa kupata zali la mentali kumpata mwanamke mwenye pesa ili ayaendeleze maisha yake, kwake, kwa jinsi alivyomwangalia Richard, alionekana kuwa naye mbalimbali kama mbingu na nchi.

Maisha yaliendelea, kila siku walikuwa watu wa kula raha. Sarafina alibadilika kwa asilimia mia moja, hakuwa yule Sarafina wa zamani, yule mshamba mshamba ambaye hata kufika Mlimani City aliogopa.

Alikuwa na bwana mwenye pesa kidogo ambaye aliyafanya maisha yake kuwa na mteremko. Hakuwa akiingia sana darasani kama kawaida, muda mwingi alikuwa akilala kwani kwa nyakati za usiku alikuwa akitoka sana na kwenda klabu.

Baada ya miezi miwili ya starehe Sarafina akaanza kuona mabadiliko, yale mapenzi aliyokuwa akiyaonyesha David yalionekana kupungua. Hakuwa mtu wa kumpigia simu kama ilivyokuwa zamani, hakuwa mtu wa kumtumia meseji kama kipindi kilichopita.

Yeye ndiye alikuwa mtumaji wa meseji na mpigaji simu. Hilo lilimuumiza kwa kuwa alikuwa akimpenda mwanaume huyo, hakutaka kumuacha, mabadiliko hayo yaliufanya moyo wake kusikia maumivu makubwa mno.

Akatafuta muda wa kukaa na David kwa lengo la kuzungumza naye lakini kila walipokutana, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa kufanya ngono. Maisha hayo yakamtawala, akawa mtumwa wa ngono kwa David kiasi kwamba hakupata muda wa kumuuliza kuhusu uhusiano wao kuanza kuyumba.

“Tatizo nini David?” aliuliza Sarafina.

“Kuhusu nini?”
“Umebadilika!”
“Nimekuwaje mpenzi? Mbona nipo kawaida. Halafu leo umetokelezea kweli! Kwa hicho kinguo ulichokivaa! Urembo wako wa asili unaonekana vilivyo,” alisema David, akamtoa Sarafina katika lengo lake. Akabaki anatabaamu.

“Huna tofauti na Jeniffer Lopez aliyokuwa kwenye ubora wake. Hebu njoo kitandani kwanza,” alisema David, hapohapo akamuinua Sarafika kutoka kwenye kochi lililokuwa chumbani kwake na kumuweka kitandani, kilichofuata ni kushikana hapa na pale, kuvuana nguo na ndani ya dakika kumi, kitanda kikaanza kulalamika.

Miezi mingine miwili baadaye, Sarafina akaanza kujihisi tofauti mwilini mwake, akaanza kusikia uchovu huku muda mwingi akitamani kulala. Hakujua ni kitu gani kiliendelea lakini hali aliyokuwa nayo alipowaambia marafiki zake, hawakumficha, wakamwambia kwamba inawezekana ikawa mimba.

Akashtuka, hakutegemea kusikia kitu kama hicho, aliogopa, japokuwa alikuwa akilala sana na David lakini hakutarajia kama ingetokea siku moja angepata mimba, aliogopa, kila alipowakumbuka wazazi wake, jinsi walivyohangaika kutafuta pesa ili asome, akaona kungekuwa na tatizo kubwa.

Hakutaka kusubiri, haraka sana akaelekea hospitalini kwenda kupima. Njiani alikuwa akitetemeka, aliogopa, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka. Hapo ndipo alipojuta kuwa na David, alijuta kuwa katika uhusiano na mwanaume huyo.

Alipofika hospitalini akakaa kwenye foleni na zamuu yake ilipofika akaingia ndani ambapo akaambiwa apeleke mkojo wake na kufanya hivyo, ulivyopimwa, akagundulika kuwa na mimba ya wiki mbili.

Alilia sana, alihuzunika kupita kawaida. Mbele yake maisha yakaanza kuonekana kuwa na ukungu mkubwa, hakuamini kama mwisho wa kila kitu ungekuwa namna ile.

Hakutaka kukaa kimya, akampigia simu David, mwanaume huyo alipoiona simu hiyo, hakuipokea, alitulia huku akiiiangalia tu. Mapenzi yalitoka moyoni mwake, hakumpenda Sarafina kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, alikuwa msichana wa starehe, alimuhitaji kipindi ambacho alikuwa na mhemko, kipindi ambacho wasichana wake wote walikuwa bize, ndipo alipopigiwa simu na kumfuata David ambapo huko, akavua nguo zake, akajilaza kitandani na kupanua miguu yake.

“Unasemaje?” lilisikika swali kutoka kwa David mara baada ya kupokea simu.

“Nataka nikuone mpenzi!”
“Kuna ishu gani?”
“Kuna kitu nataka tuzungumze!”
“Kuhusu nini?”
“Tuonane kwanza!”
“Sasa hicho kitu hakina hata intro? Niambie kwanza!” alisema David.

“Nimetoka hospitali!”
“Unaumwa?”

Hapo ndipo Sarafina akaanza kumuelezea David kila kitu kilichotokea, jinsi alivyokuwa akijisikia uchovu na kwenda hospitalini na kupima na kugundulika kwamba alikuwa na ujauzito.

“Mimba ya nani sasa?” aliuliza David.

“Yako!”
“Yangu? Eti mimba yangu! Unasema kabisa bila hofu, huogopi kudanganya mtoto wa kike, unajiamini na kusema mimba yangu,” alisema David, hakutaka kuongea sana, hapohapo akakata simu.

“Halo! Halo! Halo mpenzi!” aliita Sarafina lakini upande wa pili hakukusikika sauti tena.

Aliumia moyoni mwake, akalia kupita kawaida, hakuamini kile kilichotokea kwamba David, mwanaume aliyempenda kwa moyo wa dhati alimgeuka baada ya kumwambia kwamba alikuwa mjauzito.

Hapo ndipo alipoiona dunia chungu, hapo ndipo maneno ya wazazi wake walipomwambia kwamba alitakiwa kusoma ndipo yalipoanza kurudi kichwani mwake. Alijuta, kile kilichokuwa kimetokea kwake kilionekana kuwa kama ndoto ambapo baada ya muda angeshtuka na kujikuta akiwa kitandani.

Alimpenda David, alimwamini sana na muda mwingi walikuwa wakizungumza juu ya kutengeneza familia pamoja lakini kitu cha ajabu kabisa, alipopata mimba, mwanaume huyo akamwambia kwamba haikuwa yake.

Hakutaka kukubali, akampigia simu David kwa lengo la kumsisitizia kile alichomwambia kwamba kilikuwa ni ukweli lakini simu ya mwanaume huyo haikuwa ikipatikana na alipokuwa akipiga zaidi na zaidi, simu ikaacha kupatikana, kwa maana hiyo ikawa imezimwa.

“David….nini kimetokea? Mbona umebadilika?” aliuliza Sarafina na kuanza kulia.

Hiyo ndiyo siku iliyobadilisha maisha yake yote, huzuni kubwa ikamjaa moyoni mwake, akakosa furaha, akakosa amani, hakujua ni kitu gani alitakiwa kuwaambia wazazi wake kama tu wangegundua kuwa alikuwa na mimba.

“Sarafina! Kuna nini?” aliuliza rafiki yake aliyeitwa Catherine.

“Nina mimba!” alijibu Sarafina.

“Una mimba?”
“Ndiyo!”
“Ya nani? Ya David?”

“Ndiyo!”
“Imekuwaje? Imepitaje tena?” aliuliza Catherine kana kwamba hakujua mimba ilikuwa inapitaje.

Sarafina hakujibu swali hilo, akajilaza kitandani, akajifunika shuka na kuendelea kulia. Moyo wake ulichoma na kuchoma, aliumia lakini ukweli haukubadilika, bado uliendelea kubaki vilevile kwamba David alikataa mimba.

“Nitafanya nini? Ni lazima nimtafute!” alisema Sarafina.

Hakutaka kuchelewa, akaanza kumtafuta mwanaume huyo kwa lengo la kuzungumza naye. Hata walipokutana, hakubadilika, aliendelea kumwambia kwamba mimba haikuwa yake.

Hilo lilimuuma mno, David yuleyule aliyekuwa akimsiia ndiye aliyekuwa akimwambia maneno hayo ambayo moyoni mwake yalifanana na msumari wa moto.

Hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubaliana na ukweli kwamba alikuwa na mimba na mhusika alikataa kwa kusema kuwa haikuwa yake.

“Kaitoe,” alisema rafiki yake, Catherine.

“Bora nifanye hivyo! Siwezi kuwa na mimba, nitawaambia nini wazazi wangu! Cathy! Siwezi kuwa na mimba, sipo tayari kuzaa, ni bora niitoe,” alisema Catherine.

“Basi mwambie David!”
“Nimwambie nini?”

“Kwamba unatoa mimba!”
“Atakubali?”

“Akikataa sawa. Ila ninachotaka akupe pesa ya kutolea,” alisema Catherine.

“Sawa.”
Hilo ndilo alilolifanya Sarafina, hakutaka kuchelewa, akampigia simu David na kumwambia lengo lake la kutaka kutoa mimba hiyo hivyo alihitaji kiasi fulani cha pesa. David hakutaka kuchelewa, hapohapo, tena kwa haraka sana akamtumia kiasi cha shilingi laki mbili.

“Kaitoe haraka sana,” aliandika ujumbe mfupi.

“Sawa mpenzi!” aliitikia Sarafina na kumpanga Catherine kwamba siku inayofuata ilikuwa ni ya kwenda kwenye zahanati ya uchochoroni kwa ajili ya kutoa mimba.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa.

Comments are closed.