×

Wanafunzi Wote Hawa Wamekwenda? Inauma, R.I.P

Stori: Joseph Ngilisho | Ijumaa WIKIENDA

ARUSHA: Rest In Peace (R.I.P)! Ndivyo walivyosikika baadhi ya wananchi wa viunga mbalimbali jijini hapa jana wakiwaombea wapumzike kwa amani wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wa Shule ya Saint Lucky Vincent Nursery and Primary iliyopo Olasite waliofariki dunia kwa ajali.

Ajali hiyo iliyotokea Jumamosi iliyopita katika Kijiji cha Marera kwenye Mlima wa Rhotia wilayani Karatu wakati wanafunzi hao wakielekea kwenye ziara ya kimasomo kwenda kufanya mtihani wa ujirani mwema na Shule ya Tumaini Academy iliyopo mjini Karatu.

WIKIENDA MOUNT MERU

Walionusurika kwenye ajali hiyo ni wanafunzi wawili ambao hadi jana walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Wikienda lilifika hospitailini hapo jana kutaka kufanya mahojiano na manusura hao, lakini lilielezwa kuwa hali zao hazikuwa nzuri.

MAKANISANI HUZUNI TUPU

Pia Wikienda jana lilipita kwenye makanisa mbalimbali jijini hapa na kushuhudia waumini wakiwa kwenye huzuni, hasa akina mama huku wengine wakilia na kubembelezana kwenye vikundi.

Hata hivyo, ibada za jana nazo zilitawaliwa na maombi juu ya tukio hilo ambapo wote waliofikwa na tukio waliombewa wawe na ujasiri katika kipindi kigumu walicho nacho.

Katika tukio hilo, ilielezwa kwamba basi hilo walilopata nalo ajali aina Toyota Coaster lilikuwa kati ya mabasi matatu ya shule hiyo yaliyokuwa yameongozana na taarifa kutoka eneo la tukio zilieleza kuwa basi hilo lilikuwa katikati ya mengine.

NINI CHANZO CHA AJALI?

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wakati basi hilo linapita mji mdogo wa Rhotia Hill lilikuwa katika mwendo mkali bila kujali wingu zito lililokuwa limetanda na mvua iliyokuwa ikinyesha huku barabara ikiwa na utelezi kutokana na aina ya udongo wa eneo hilo ambao ulikuwa umeingia barabara pamoja na kwamba ni barabara ya lami.

Inaaminika kuwa, udongo huo ndiyo ulifanya tairi kuteleza hivyo kukatika kwa breki kwenye mteremko huo mkali ambao pia kuna daraja.

Walidai kuwa, basi hilo lilikuwa linashuka kwa kasi kwenye mteremko mkali wa Mlima Rhotia katika makutano ya Barabara ya Kwa-Karani huku wanafunzi hao wakipiga kelele za kuomba msaada.

Mashuhuda hao walisema walishangaa kuona basi hilo likipaa na kutumbukia katika korongo refu la Mto Marera unaopatikana wilayani Karatu na kusikika kishindo kikubwa ndipo watu wa eneo hilo wakakimbilia na kuanza kutoa msaada.

29 PAPOHAPO

Walidai kuwa, wanafunzi 29 walifariki dunia papohapo pamoja na walimu wao wawili na dereva wa gari hilo hivyo kufanya idadi ya waliokufa wakati huo kuwa 32 huku majeruhi wakikimbizwa katika Hospitali Teule ya Wilaya Karatu na Kituo cha Afya cha Rhotia kabla ya kuhamishiwa Mount Meru.

MADEREVA WA WATALII

Madereva wazoefu wa barabara hiyo na eneo hilo lenye mlima mkali, kona kali na mteremko mkali ambao hufanya safari za kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama wanalisimulia kuwa eneo hilo huwa linataka madereva wazoefu na mwendo wa kawaida chini ya spidi 40 kwa saa.

Walisema kuwa, ni eneo ambalo dereva anatakiwa kuwa makini mno na kwa dereva asiyekuwa mwangalifu, lolote linaweza kutokea.

KAMANDA WA POLISI

Akizungumza na Wikienda jana juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Charles Mkumbo alisema kuwa, bado polisi wanachungunza chanzo cha ajali hiyo na taarifa itatolewa kwa umma uchunguzi huo utakapokamilika.

VILIO, ULINZI MOUNT MERU

Katika Hospitali ya Mount Meru ambapo kulitawaliwa na vilioambapo viongozi wa serikali na wa kisiasa walionekana walifika kuonesha kuguswa na tukio hilo.

Kwenye la mochwari kulifurika watu ambao walikuwa wakisubiri kuona na kutambua miili ya wapendwa wao hivyo kuwalazimu polisi kuimarisha ulinzi.

SHULE YAFUNGWA

Taarifa zilizopatikana jana zilieleza kuwa shule hiyo ilifungwa kwa siku saba kwa ajili ya maombolezo ya vifo hivyo.

MKUU WA SHULE SASA

Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa shule hiyo, Ephraim Jackson alisema kuwa hadi jana jioni idadi ya waliofariki ni 36 huku wanafunzi wawili, Sadiely Ismail na Wilson Tarimo wakiwa mahututi katika Hospitali ya Mount Meru.

Leo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu, kwa niaba ya Rais Dk John Pombe Magufuli ataongoza kazi ya kuaga miili hiyo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

BAADHI YA WALIOFARIKI DUNIA

Baadhi ya majina ya ya waliofariki dunia yaliyopatikana kwa msaada wa walimu wa shule hiyo ni pamoja na Mteage Amos, Justine Alex, Irene Kishari, Gladness Goodluck, Praise Roland, Shadrack Biketh, Junior Mwashuye, Aisha Said, Oumligh Herri Rashid, Gema Gerald, Rebecca Daudi, Hagai Lucas, Said Ally na Ruth Ndemna.

Wengine ni Atusa Kassim, Neema Eliwashi, Neema Martine, Greyson Robson Masana, Heavennight Enock, Ian Tarimo Anold Alex, Naomi Hosea, Rukia Altam, Eliapendo Elihudi, Marion Mrema, Rehema Msuya, Sabrina Said na Prisca Charles.

 

Arusha Ilivyozizima Miili ya Wanafunzi Waliokufa kwa Ajali Ikiagwa

Leave a Comment