Elice Mwakanjila Aibuka Kidedea Miss Ustawi 2017
MWANAFUNZI wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Elice Mwakanjila usiku wa kuamkia leo Jumamosi, ameibuka kinara wa Miss Ustawi 2017, baada ya kufanya vyema na kuwapiku wenzake 10 aliokuwa akishindana nao kugombania taji hilo.
Ishu nzima ya tukio hilo ‘ilihapeni’ katika Ukumbi wa King Solomon, Namanga jijini Dar ambapo Elice alichaguliwa kuwa mshindi baada ya kufanya vyema kwenye vipengele vya kusakata rhumba, kutoka na vazi la ufukweni na kumaliza shoo na vazi la jioni.
Elice alichaguliwa kuwa kinara wa wenzake na orodha ya majaji wakiongozwa na Jaji Mkuu, Happiness Watimanywa. Ruth Deogratius akibeba nafasi ya pili na nafasi ya tatu ikichukuliwa na Melody Thomas.
Katika shindano hilo mgeni rasmi alikuwa Mstahiki Meya wa Kinondoni, Benjamini Sitta, ambaye aligawa vyeti kwa baadhi ya wadhamini waliokuwa wakiliwezesha shindano hilo na miongoni mwa wadhamini hao ni Gazeti Pendwa la Amani linalochapishwa Kampuni ya Global Publishers ltd na kuwa mitaani kila Alhamisi. Cheti hicho kilipokelewa na mwandishi wa gazeti hilo, Musa Mateja.
(PICHA: MUSA MATEJA/GPL)