×

Fainali Sportpesa Super Cup Leo Dar …Global TV Online Tutakuwa Live

 

Timu za Gor Mahia na AFC Leopards zinatarajia kukutana leo Jumampili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa fainali wa michuano ya SportPesa Super Cup.

Timu hizo zimetinga fainali baada ya Gor Mahia kuitoa Nakuru All Stars ya Kenya kwa mabao 2-0 katika nusu fainali huku AFC Leopards ikiitoa Yanga kwa penalti 4-2 katika hatua hiyo Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru.

Zinapokutana timu hizo za mji mmoja mchezo wao huwa unajulikana kwa jina la Nairobi Derby au Mashemeji Derby.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwani timu hizo zinaupinzani wa jadi hivyo siyo rahisi kutabiri upande gani unaweza kuibuka na ushindi.

SUBSCRIBE NOW: https://www.youtube.com/user/uwazi1

Gor Mahia wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa hawajaruhusu hata bao moja kwenye nyavu zao wakati AFC Leopards, wakiruhusu bao moja walilofungwa kwenye mchezo wa ufunguzi dhidi ya Singida United mbali na hapo timu hiyo imekuwa ikitegemea mikwaju ya penalti ili kupata ushindi.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Medie Kagere ndiyo anatakiwa kuchungwa zaidi kwa mabeki wa AFC Leopards kwani ameshaifungia timu yake mabao matatu kwenye michuano hiyo inayofikia tamati hapo kesho.

Kocha wa Leopards, Dennis Kitambia ambaye ni raia wa Tanzania, amesema anawaheshimu Gor Mahia kwakuwa ni timu kubwa lakini wamejpanga kuhakikisha wanacheza vizuri na kutwaa taji hilo.

Kitambi amesema anatambua uwezo wa wapinzani wao Gor Mahia, na walishapoteza mechi mbili zilizopita za kwenye ligi hivyo watajitahidi kuhakikisha mchezo huo wanashinda na kulipa kisasi.

“Tulifungwa mabao 3-0, kwenye mchezo wa ligi kwa hiyo mchezo wa kesho ni nafasi nzuri kwetu kuweza kulipa kisasi, najua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu ya kufahamiana lakini kama tutacheza kwa nidhamu hakuna kitakachoshindikana,” amesema Kitambi.

Kwa upande wake Kocha wa Gor Mahia, Zedekiah Otieno, amesema anauhakika mkubwa wa kutwaa taji hilo kufuatia ubora wa kikosi chake ukilinganisha na timu ambayo wanakwenda kucheza nayo.

Otieno amesema ni mchezo mzuri na wenye upinzani  hivyo watacheza kwa kujituma ili kuhakikisha wanamaliza vizuri kwa kushinda michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza Tanzania.

“Leopards ni timu nzuri tangu imekuja huku imeweza kucheza vizuri na kuonyesha mabadiliko najua mchezo utakuwa mgumu lakini naamini baada ya dakika 90 tutaibuka washindi,” amesema Otieno.

Bingwa wa michuano hii iliyoanza Juni 5, mwaka huu atapewa zawadi ya dola 30,000 (Sh milioni 66.9 za Kitanzania) na nafasi ya kucheza dhidi ya Everton ya England, Julai 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Leave a Comment