
Tawi la timu ya soka ya Simba jijini Mwanza, Simba Mwanza Task Force imemkabidhi tuzo ya heshima nahodha wa timu hiyo Jonas Mkude katika hafla iliyofanyika ukumbi wa The Joint uliyopo Isamilo jijini Mwanza.
Wanachama wa tawi hilo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bittony Mwakisu pamoja na Katibu, Filbert Kabago wamesema wameona wamemkabidhi tuzo hiyo Jonas Mkude kutokana na kuridhishwa na mchango wake katika Timu ya Simba.
Akikabidhi tuzo hiyo Mgeni Rasmi wa Hafla hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, Wilbert Chuma, alimpongeza Mkude na kumtakia maandalizi mema kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara pamoja na mashindano ya Kimataifa.
“Kwanza nakupongeza sana kwa hapa ulipofikia lakini pia hiki ulichokipata kwa kutolewa na wanachama hawa ni kwa kutambua mchango wako uwanjani na tunakutakia maandalizi mema ya msimu ujao,” alisema Chuma.
Ikumbukwe kwamba msimu uliomalizika Mwezi Mei, Mkude akiwa Nahodha wa timu ya Simba aliisaidia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.
Lakini pia aliiwezesha Timu yake kucheza fainali ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar walipofungwa na Azam kwa bao 1-0, na mbali na hilo pia kutwaa ubingwa wa Kombe la Azam Sports Federation kwa kuwachapa Mbao FC mabao 2-1.
Simba kwa kutambua Mchango wake wameamua kumuongezea mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Miamba hiyo ya Soka kutoka mtaa wa Kariakoo Msimbazi Jijini Dar es Salaam.
Na Johnson James | Global TV | Mwanza