
KWA mbali, ukimtazama unaweza kudhani unakutana na Hasheem Thabeet, yule kijana wa Kitanzania aliyekuwa akicheza Ligi ya Kikapu ya Marekani, NBA, kwenye timu kadhaa ikiwemo Oklahoma City Thunder.
Lakini huyu siyo Hasheem bali ni Julius Charles ambaye amejipatia maarufu mkubwa kupitia promosheni ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, akijulikana kama Mr Shinda Nyumba.
Ana urefu wa Futi 7 na inchi 5, mrefu zaidi ya mcheza kikapu huyo wa Marekani mwenye urefu wa futi 7 kamili.
Alizaliwa Geita wilayani Chato miaka 20 iliyopita, akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto saba. Kwa mujibu wa mama yake, alizaliwa akiwa mrefu na uzito wa kilo tatu.

KATIKA FAMILIA YENU KUNA MREFU MWINGINE ZAIDI YAKO?
Hapana ni mimi peke yangu ndiye mrefu, ndugu zangu wengine wote wana vimo vya kawaida, hata wazazi wangu pia wako kawaida, ila mama yangu hunieleza marehemu babu yangu alikuwa mrefu ingawa siyo urefu mkubwa kama wangu.
VIPI KUHUSU ELIMU YAKO?
Nimesoma Shule ya Msingi Mlimani iliyopo mkoani Mwanza, sekondari nimesoma shule ya vipaji ya Power Memorial High School kidato cha kwanza hadi cha nne na kwa sasa nipo kidato cha tano Shule ya Mesac Open iliyopo Mwenge.

CHANGAMOTO GANI UNAZIPITIA KUTOKANA NA UREFU WAKO?
Mwanzoni nilikuwa najisikia vibaya sana, na niseme tu kwa miaka mingi nimekuwa ni mtu mwenye hasira kutokana na jambo hilo, hata hivyo tangu nijiingize kwenye mchezo wa mpira wa kikapu nimejikuta changamoto hiyo inazoeleka moyoni mwangu.
Vilevile kila ninapopita watu wengi wanapenda kupiga picha na mimi kitu ambacho sasa kinakuwa ni karaha.
MSOSI WAKO UPOJE?
Nikipata kilo moja ya unga kwa ajili ya ugali, nikila ndiyo nashiba, na ukweli ni kwamba chakula ninachokipenda ni ugali wa dona na samaki.
SHINDANO LA SHINDA NYUMBA PAMOJA NA JINA LAKO LA UTANI LA MR SHINDA NYUMBA UNALICHUKULIAJE?
Kwanza niseme naishukuru Global Publishers kwani ukiachilia mbali mchezo wa mpira wa kikapu ambao umenifanya niwe na furaha, lakini pia Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba imenifanya furaha yangu na faraja iongezeke zaidi, nimeizoea zaidi jamii yangu ambayo awali nilikuwa naigopa, natamani hili shindano lingekuwa kila siku maana limenibadilisha mno kifikra.
UNAUMUDU KWA KIWANGO GANI MCHEZO WA MPIRA WA KIKAPU?
Ninaumudu vizuri sana, nina uwezo mzuri wa kufunga mabao mengi vile ninavyotaka kwa kuwa urefu wangu umekuwa ukinisaidia, timu yangu ya Street Worries mimi ni mchezaji wa kutegemewa.
USHAWAHI KUJIINGIZA KWENYE UHUSIANO WA KIMAPENZI?
Bado, kwa sasa akili yangu haipo hata kidogo kwenye mambo hayo, kwa kuwa bado nasoma.
MCHEZAJI GANI WA KIKAPU ANAYEKUVUTIA?
Kwanza napenda nifuate nyayo za Hasheem Thabeet, lakini kwa mchezaji anayenivutia ni LeBron James.
UNA UJUMBE GANI KWA WATANZANIA?
Kwanza napenda watu wanione mimi ni binadamu wa kawaida kama wao, tofauti yangu na wao ni mrefu wa kimo tu, kwa hiyo wasinishangae sana.
Ally Katalambula| Dar es Salaam