×

VIDEO: Alichokizungumza Tundu Lissu Baada ya Kuachiwa na Polisi

Tundu Lissu.

 

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo muda mfupi baadaye, amefanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza msimamo wake na kufafanua kuhusu sakata la polisi kutaka kumpima mkojo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amempa dhamana Lissu leo, Julai 27 akisema upande wa mashtaka umeshindwa kutaja kesi ambayo mshtakiwa huyo wa kesi ya uchochezi aliwahi kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa.

Amesema hoja ya upande wa mashtaka kuwa Lissu anyimwe dhamana kwa ajili ya usalama wake haijajitosheleza kumweka ndani.

Hakimu Mashauri amesema kundi la mawakili 18 wamejitokeza kumwakilisha Lissu, hatua inayoonyesha watu wana upendo dhidi yake.

Kutokana na hayo, Hakimu Mashauri ametoa dhamana akimtaka Lissu kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao watasaini bondi ya Sh10 milioni kila mmoja.

Pia, amemtaka asitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.
Saa 3:50 asubuhi, baada ya kukamilisha masharti ya dhamana Lissu aliingia kwenye gari lake na kuondoka eneo la Mahakama ya Kisutu.

Lissu leo amewakilishwa na wakili Peter Kibatala kwa niaba ya mawakili wengine. Kesi yake inatarajiwa kuunguruma tena Agosti 24, mwaka huu.

 

Alichokizungumza Tundu Lissu Baada ya Kuachiwa na Polisi kwa Dhamana

Leave a Comment