×

Kabila Linalohusudu Vitambi, Linalotembea Utupu-7

Wanawake wa Kabila la Bodi wakisukana.

 

WIKI iliyopita tuliona jinsi wavulana wa Kabila la Bodi wanavyokuzwa kwa kufundishwa kazi mbalimbali ikiwemo ya kulinda mifugo yao.

Tuliona jinsi wanavyofundishwa na wazee wao jinsi ya kukimbia wakiwa juu ya migongo ya ng’ombe kwa nia ya kuilinda mifugo yao, Endelea:

Leo tuwaangazie wanawake wa kabila hilo. Wengi ni weusi tii, ni nadra sana kuwaona wanawake au hata wanaume weupe au maji ya kunde.

Tofauti na makabila mengine ambayo wanaume huwa moja ya kazi zao ni kujenga nyumba, watu wa jamii ya Bodi wanaojenga nyumba za kuishi familia huwa ni wanawake.

Ujenzi wa nyumba hizo hujengwa kwa kushirikiana kati ya koo na koo, ambapo wanawake walioalikwa kufanya kazi hiyo baada ya kazi, yaani jioni huburudishwa kwa kunywa pombe iliyoandaliwa na mwanamke aliyekuwa akisaidiwa kujenga nyumba.

Nyumba huwa ni ya vijiti na kutoka kijiti hadi kijiti hufungwa kamba ambazo huchunwa kwenye miti maalum inayojulikana kwa kutoa kamba.

 

Wanaume wakiwa kwenye mashindano ya vitambi.

 

Vijiti hivyo huchimbiwa kwenye mduara kulingana na ukumbwa wa nyumba na baada ya kazi ya kuunganisha vijiti kwa kutumia kamba kwisha, hufunikwa kwa nyasi.

Wavulana waliovunja ungo ni marufuku kuingia kwenye nyumba zilizojengwa na mama zao, badala yake wao

huruhusiwa kujenga zao ndogo pembeni, mita kama ishirini au zaidi kutoka nyumba ya wazazi.

Watu hawa hawana vitanda na badala yake hutumia ngozi ya mbuzi kutandika juu ya ‘magodoro’ yaliyotengenezwa kwa kamba au magome maalum ambayo huchunwa kwenye miti na kupondwa pondwa kisha kutengeneza godoro ambalo hutandikwa ngozi.

Nje ya nyumba zao hakuna viti, hutumia magogo kwa wanaume au ngozi laini ya mbuzi kwa akina mama na watoto kukalia wanapokuwa nje ya nyumba zao.

Moto wao hupatikana kwa wanaume au hata wanawake kupekecha miti maalum ambayo hutoa moto na kukolezwa baada ya kuegeshwa vumbi linalotoka kwenye nyasi maalum laini ambazo hushika moto haraka.

Wanaume huutumia moto kutengeneza michale kwa kuchoma chuma na kukipondaponda kisha kutengeneza mishale, panga, mundu au kisu kwa ajili ya kazi zao mbalimbali.

Mashindano ya vitambi.

 

Mara nyingi utengenezaji wa mishale huenda sambamba na uundwaji wa pinde na licha ya kuwa na mifugo, hutumia silaha hizo kuwindia wanyama au kuwaua maadui wa mifugo yao kama vile simba au chui.

Kwa kawaida Wabodi wanaume huwa hawatembei na mapanga badala yake silaha hizo hutumika na akina mama kwa ajili ya ujenzi au kukatia kuni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Wanaume mara nyingi huwa na mishale iliyotengenezwa kienyeji na huwa inatiwa sumu ili kurahisisha kuwaua wanyama wakali.

Mishale hiyo haiwekwi hovyo kutokana na sumu iliyopakwa kwani kama inamchoma binadamu anaweza kupoteza maisha.

Akina mama wao kazi yao kubwa ni kuwapikia chakula waume zao na watoto. Na huhakikisha chakula kinakuwepo kwani wao ndiyo hufuata kwa wakulima kununua baada ya kuuza maziwa na mifugo kwa ruhusa za waume wao.

Majiko yao huwa ni ya mafiga matatu kama zilivyo familia nyingi za Kiafrika japokuwa wakati wa sherehe maalum ambayo huchinjwa mifugo, moto huandaliwa na wanaume ambao hubanika nyama zikiwa kwenye mstari.

Chumvi wanayo ya kienyeji ambapo wanawake huwa wanakwenda sehemu maalum ambazo zina chumvi chumvi na kuchimba mchanga ambao huchujwa majumbani kwa kutumia maji, maji hayo yakichemshwa, hutoa chumvi ya kienyeji.

Wasichana wao waliobalehe huishi kwa masharti magumu sana.

Je, ni masharti gani hayo? Usikose kufuatilia makala haya Jumanne ijayo hapahapa.

NA MWANDISHI WETU NA MITANDAO

Leave a Comment