
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshutumu masharti mapya yaliyotolewa na serikali kuhusu utoaji mikopo kwa wenye kutaka kujiunga na elimu ya juu.
Hayo yalisemwa leo na Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo, alipozungumza na waandishi wa habari akisema kwamba masharti hayo ni makali, magumu na ya kibaguzi kwa idadi kubwa ya watoto wa familia maskini.
Alitoa mfano wa sharti kwamba watoto ambao wazazi wao wanahusika katika kujaza fomu za maadili ya uongozi hwaruhusiwi kuomba mikopo hiyo. Akifafanua, alisema madiwani ni watu wenye kipato cha chini cha posho ya sh. 300,000 kwa mwezi, hivyo kuwanyima watoto wao fursa ya kupata mikopo ni kuwabagua bila msingi.
Alisemea pia juu ya wazazi wenye miradi au biashara zinazotambuliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), watu wenye umri unaozidi miaka 30, na watu waliomaliza kidato cha sita au diploma kwa zaidi ya miaka mitatu nyuma, ambao nao hawaruhusiwi kupata mikopo.
Lyimo alisisitiza pia nia ya chama chake kwamba pindi kiingiapo madarakani kitahakikisha kinatoa elimu bure na bora bila ya kuhusisha masharti magumu kwa watu wanaotaka kujiunga na elimu ya juu.