Klabu ya Simba leo imefanya mazoezi yake ya mwisho kuelekea mchezo wa Ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Mchezo wa Ngao ya Jamii) dhidi ya wapinzani wao Yanga SC utakaopigwa kesho Jumatano, Agosti 23 kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Global Publishers imewashuhudia Simba wakijifua katika Uwanja wa Boko huku wachezaji hao wakiwa na ari nzuri ya kuwakabili wapinzani wao kesho.
Mchezo huo wa aina yake unatarajiwa kuwa naupinzani mkubwa kama ambavyo imekuwa desturi ya timu hizi kubwa hapa nchini zikikutana, huku vituko mbalimbali vya mashabiki vikitarajiwa kuonekana uwanjani.
Michezo ya Ngao ya Jamii, kwa kawaida huwa ni ‘Super Cup’, kwa maana ya kukutanisha mabingwa wa michuano miwili tofauti (au bingwa wa FA vs mshindi wa pili wa ligi kama bingwa wa ligi na FA ni yuleyule) lakini kwa muda mrefu kwa Bongo imekuwa ikimkutanisha mshindi wa kwanza na wa pili wa ligi kuu kwa kuwa hatukuwa na Kombe la FA, hivyo kukosa mantiki.
Safari hii kuna uhalisia zaidi, watu wataona nani mkali kati ya bingwa wa ligi kuu (Yanga) na wa Kombe la FA (Simba).
Kwa Tanzania, hii ni itakuwa ni mechi ya 10 ya Ngao ya Jamii, tangu ilivyoanzishwa mwaka 2001, kisha ikafa na kuja kuibuka tena baada ya miaka nane.
Simba walitua jana kutokea Zanzibara wakati Yanga wao wanatarajiwa kutua Dar leo Jumanne wakitokea visiwani humo walikokuwa wameweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo huo.
NA MUSA MATEJA | GPL