







KAMPUNI ya Aborder inayojishughulisha na masuala ya uuzaji wa bidhaa za Solar, televisheni za kisasa, redio, majiko ya kupikia na bidhaa zingine zitumiwazo majumbani, imezindua msimu mpya wa uuzaji wa bidhaa mpya na za kisasa.
Uzinduzi huo ulifanyika usiku wa jana katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam kwa kwa maonyesho ya bidhaa hizo ambazo huingizwa sokoni kila mwaka kwa ujio na muonekano wa tofauti. Hafla hiyo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo wateja wa bidhaa hizo.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Billy Deng, alisema: ‘’Msimu uliopita tuliahidi kuwaletea bidhaa mpya na zenye ubora zaidi ili kuendana na mahitaji ya jamii lakini pia ikiwa ni njia ya kuboresha soko na kuwajali wateja wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono. Hivyo nawaomba mzipokee bidhaa hizi bora kabisa na zenye kiwango cha kimataifa.
“Tutaendelea kuungana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Magufuli kwa kuja na kasi ya kuongeza viwanda hapa nchini kwani tayari tumeshaanza kumiliki kiwanda cha kutengeneza misumari kilichopo mkoani Pwani, ambacho kwa hakika kinazalisha misumari yenye ubora na kiwango chenye kuhitajika.”
Mbali na uzinduzi wa bidhaa hizo, kampuni hiyo ilikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 17 kwa taasisi ya kulea watoto yatima ya Neema iliyoko wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kusaidia kuendesha kituo hicho, ikiwa ni njia ya kurejesha kwa jamii kidogo wanachokipata.