




WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dk Hussein Mwinyi, leo amewaongoza waumini wa Kiislamu katika kusherehekea Sikukuu ya Eid El Hajj ambayo ni maarufu kama ‘Eid ya Kuchinja’.
Hafla hiyo imefanyika kwenye Viwanja vya Masjid Taqwa, Ilala-Bungoni jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 1:30 asubuhi ambapo ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa, Mufti Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuberi na viongozi wengine wengi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwinyi amesisitiza suala la amani kwa Watanzania wote huku akiwataka waumini kubadilika na kuondokana na dhana zote potofu zisizokuwa na manufaa katika kulijenga taifa chini ya Rais John Magufuli.
Kwa upande wa Mufti Mkuu wa Tanzania, Zuberi amewatakia Waislamu kote nchini na wananchi kwa jumla sikukuu njema ya Eid El Hajj na kumtaka kila mmoja kusherehekea kwa utulivu na mshikamano.
Pia amewataka walimu wa shule za Kiislamu za madrasa kote nchini kuhakikisha wanawaelimisha wanafunzi wao ili waweze kuwa na maadili mema na si kuwapatia elimu ya dini yao tu, bali wafundishwe pia masomo mbalimbali ili kuwawezesha kuwa na maadili mema na utaalam unaotakiwa katika maisha yao ya baadaye na kuwa viongozi bora.
Mufti alitoa miezi sita kwa taasisi iliyokuwa na jukumu la kuwasafirisha mahujaji kwenda Makka na kushindwa kufanya hivyo, irudishe fedha ilizokuwa imezichangisha kutoka kwa waumini waliotegemea kwenda huko.
Alisema waumini hao wataweza kwenda kuhiji huko Makka mwaka kesho na kwamba uongozi wake utahakikisha tatizo kama hilo halitajitokeza tena na kuathiri safari za mahujaji.
NA DENIS MTIMA/GPL