×

George Majaba Amenunua Nyumba kwa Sh. 59,500 Tu!

UKISIKIA kismati ndiyo kama hiki. Mshindi wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba, ambaye ni mkazi wa Makole, Makao Makuu ya Nchi, Dodoma, ni sawa na kuwa ameinunua nyumba yake hiyo mpya, yenye thamani ya mamilioni ya shilingi, kwa kiasi kidogo cha shilingi elfu hamsini na tisa tu na mia tano (59,500).

Katika mahojiano na gazeti hili wiki iliyopita, Majaba, ambaye ni kondakta wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Dodoma Mjini na Vijijini, alisema alikata jumla ya kuponi 119 za gazeti la Championi kwa nyakati tofauti, ndani ya miezi sita ya uhai wa shindano hilo lililoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers.

“Mimi ni msomaji mzuri wa magazeti ya Global, nimekuwa nikisoma kwa zaidi ya miaka 15, mara nyingi huwa sikosi magazeti yenu, hasa ya michezo kwa kuwa mimi ni mdau mzuri wa michezo.

“Shindano hili lilipoanza nikawa nakusanya magazeti na kujaza kuponi, nilikuwa nakusanya huku naendelea kufanya kazi zangu.

“Mimi ni kondakta wa mabasi yanayotoka hapa Dodoma yanaelekea vijijini maeneo kama Dabalo.

“Mara ya kwanza nilikusanya kuponi 73 nikazituma huko Dar, mara ya pili nikakusanya kuponi 46, sasa siku ya kuzituma kuna baadhi nilikuwa sijazijaza, nikaenda nazo Posta kwa ajili ya kuzituma, kufika nikawa nazijaza nikiwa hapohapo Posta, sasa wakati naendelea wakaniambia wanataka kufunga na kuzisafirisha, nikawa nazijaza harakaharaka.”

“Kuponi zote nilikuwa najaza namba ya simu, nadhani haraka ya kujaza siku hiyo ndiyo nikasahau kujaza namba katika hiyo kuponi niliyoshinda.

“Sasa Jumatano iliyopita nilirudi nyumbani mapema, nikawa nasikiliza michezo kwenye simu nikiwa nje ya pale Makole ninapokaa, hiyo nyumba nimepanga.

“Watoto wakanifuata na kuniambia wamepigiwa simu kuwa nimeonekana Channel Ten, natafutwa Dar nimeshinda nyumba, nikashangaa sana na kujiuliza mbona sijapigiwa simu, baadaye simu zikaanza kupigwa nyingi kwangu kwa watu wanaonifahamu hadi ikazima chaji,” alisema Majaba.

Nakala ya gazeti moja la Championi linauzwa kwa shilingi mia tano, sawa na magazeti mengine ya Global Publishers ambayo ni Ijumaa Wikienda, Uwazi, Risasi na Amani.

Kwa maana hiyo, nakala 119 ambazo msomaji huyo alitumia kununua magazeti hayo, ni sawa na shilingi 59, 500 tu, ambazo zimemuwezesha kujipatia nyumba hiyo yenye thamani ya mamilioni ya shilingi, ambayo ina samani zote za kisasa ndani.

Nyumba hiyo iliyojengwa eneo la Bunju B nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ina vyumba vitatu, ikiwemo Master Bed Room, jiko, chumba cha chakula, maongezi, choo na bafu.

Kana kwamba haitoshi, mmiliki huyo mpya, atakabidhiwa nyumba ikiwa tayari imeshaunganishwa nishati ya umeme.

Katika Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Kwanza, Nelly Mwangosi, Mkazi wa Iringa Mjini, aliibuka mshindi wa nyumba iliyojengwa Salasala, nje kidogo ya jiji la Dar.

 Stori: Mwandishi Wetu

Leave a Comment