
Walichanganyikiwa, ilikuwaje muuaji wa Belleck awe yule msichana aliyefanya mauaji kule nchini Misri na wakati mtu huyo alikuwa akitafutwa kila kona nchini humo?
Alishangaa. Hakutaka kutulia, haraka sana akatafuta namba ya simu ya mkuu wa polisi nchini Misri kupitia kitengo cha Interpool na kumuuliza kuhusu suala lile kama muuaji alikamatwa au la.
“Bado hatukumkamata!”
“Basi sawa.”
“Kuna nini?”
“Amefanya mauaji na huku pia.”
“Amefanya mauaji! Lini?”
“Leo hii!”
“Haiwezekani! Hakuna mtu anayeweza kuua kirahisi, ndani ya siku chache kama hizi,” alisema polisi mkuu kutoka nchini Misri.
“Ndicho kilichotokea! Ila nahisi tutampata japokuwa swali moja muhimu la kujiuliza, hivi kwa nini anaua mabilionea tu?” aliuliza polisi wa Ufaransa.
“Mmh! Kweli! Napata picha! Kwa nini mabilionea? Hii inamaanisha ndani ya siku chache zijazo kutakuwa na bilionea mwingine atauawa kama tu tusipofanya kazi ya ziada kumkamata?”
“Inawezekana! Hebu tusubiri. Ila nina uhakika kwa mauaji aliyoyafanya hapa, tutamkamata! Tena wiki hiihii na atatuambia kwa nini anauacha ujumbe huu kila anapofanya mauaji,” alisema polisi wa Ufaransa na kukata simu. Msako wa kumtafuta mwanamke huyo ukaendelea.
****
“Where is the father?” (padri yupo wapi?) alisikika msichana mmoja akiuliza kanisani alipokwenda kwenye chumba kidogo kwa ajili ya kuzungumza na padri lakini bahati mbaya hakumkuta.
“He was right there,” (alikuwa huko)
“Where?” (wapi?)
Watu walikuwa wakiulizana kanisani. Hakukuwa na watu wengi, kanisa zima lilikuwa na washirika watano ambao walikaa kwa kujigawa ndani ya kanisa hilo kubwa.
Walishangaa, kitendo cha kutokumuona padri kanisani humo kiliwapa wakati mgumu wa kutokugundua mwanaume huyo alikuwa wapi kwani kwa siku kama hiyo, tena ya kuungama dhambi zao, ilikuwa ni lazima padri awepo ndani ya chumba kile cha kuungamia dhambi.
Hakukuwa na mtu aliyejua mahali alipokuwa ila hawakuwa na hofu hata kidogo kwani waliamini kwamba padri huyo angerudi kanisani hapo na mambo kuendelea kama kawaida.
Hilo lilikuwa kanisa kubwa jijini New York nchini Marekani. Watu wengi wa Kanisa la Roma walikuwa wakishiriki misa katika kanisa hilo kubwa, wengi walitoka nchini nyingine na kufika katika kanisa hilo ambalo lilikuwa la kwanza kutembelewa na Papa José Kentenich miaka ya 1880.
Siku ya kwanza ikapita lakini hakukuwa na mtu aliyefahamu mahali padri alipokuwa. Walikuwa wakishiriki misa lakini kanisa liliongozwa na padri msaidizi ambaye naye hakujua mahali padri mkuu alipokuwa.
Wakati siku ya tatu ikiwa imeingia ndipo kanisani kukaanza kusikika harufu mbaya. Ilikuwa ni harufu ya mzoga iliyokuwa ikiwasumbua, wengi walihisi kwamba inawezekana mzoga huo ulikuwa nje ya kanisa hilo lakini kila walipokaa, wakajua kabisa mzoga huo ulikuwa ndani ya kanisa hilo.
Hapo ndipo walipoanza kuchunguza, waliangalia huku na kule na mwisho wa siku kugundua kwamba mzoga huo ulikuwa ndani ya chumba kile cha kuungamia dhambi ambacho kiliruhusiwa kuingiwa na mtu mmoja tu ambaye ndiye padri.
Hawakuwa na jinsi, kwa kuwa hiyo ilikuwa ni siku ya tatu bila padri kuonekana, wakazunguka upande wa nyuma na kuingia. Walichokutana nacho kiliwashtua kupita kawaida, waliiona maiti ya padri ikiwa sakafuni, ilikuwa imechomwa visu kadhaa shingoni na ubavuni huku ikianza kuharibika na kuutoa harufu mbaya na kali.
Picha iliyoonekana mahali hapo iliwasisimua sana kwani mbali na kuuawa, ilionekana kabisa kwamba mwili wake uliburuzwa na hivyo kuacha alama za michirizi ya damu kitu kilichowafanya kusisimka zaidi.
“Mungu wangu! Padri!” alisema jamaa mmoja huku akionekana kushtuka.
“Jamani! Nini kimetokea?” aliuliza msichana mmoja, naye mwenyewe kama alivyokuwa mwanaume yule, alichanganyikiwa.
Walichokifanya ni kupiga simu katika kituo cha polisi hapo New York katika Mtaa wa Brooklyn ambapo baada ya dakika kadhaa polisi wakafika na kwenda ndani ya chumba kile.
Harufu iliyokuwa ikitoka humo ndani, iliwashtua, ilikuwaje mtu afe ndani ya chumba halafu ichukue siku nyingi kiasi hicho mpaka kugundua, wakahisi kwamba kulikuwa na tatizo.
“Nani amefanya mauaji haya?” aliuliza polisi mmoja.
“Hatujui! Tulikuwa tukimtafuta sana padri lakini hatukumpata mpaka leo hii tumeuona huu mwili wake,” alisema mwanaume mmoja.
Mwili ukapigwa picha, polisi walihakikisha wanafanya taratibu zote zilizotakiwa kufanywa na wao kisha kuuchukua mwili kwa lengo la kuondoka nao. Wakati wakiwa wameutoa mahali pale, wakakiona kipande cha karatasi pembeni yake, wakakichukua na kuanza kukisoma, kilikuwa kidogo kilichoandikwa maneno machache yaliyosomeka ‘It is done’ kwa maana ya kazi kukamilika.
Polisi walivyokiona kipande hicho cha karatasi walishtuka, hawakuamini kama kweli muuaji aliyekuwa amefanya mauaji katika nchi mbili, Misri na Ufaransa ndiye ambaye alifanya mauaji ndani ya kanisa hilo.
Wakapeana taarifa kwa njia ya simu kwamba kulikuwa na mauaji mengine yaliyokuwa yamefanyika na muuaji alikuwa yuleyule aliyeua kipindi cha nyuma kitu kilichowafanya watu wengi wawe na hofu juu ya muuaji huyo.
“Huyu ni nani?” aliuliza polisi mmoja, kwa jinsi muuaji huyo alivyoonekana kuwa hatari katika kufanya mauaji, wengi wakahisi kwamba alikuwa mwanaume aliyepitia mafunzo makubwa ya kuua na kuficha siri ya mauaji yake.
Baada ya kifo cha Padri Mathew Luke kutangazwa, watu hawakuamini kile walichokisikia. Mauaji yake yalifanana na mabilionea ambao waliuawa kipindi cha nyuma hivyo kuifanya dunia ishangae na kutaka kujua sababu ya muuaji kufanya mauaji hayo.
Kila kona gumzo lilikuwa juu ya muuaji huyo, watu hawakukubali, walitaka kupata ukweli kwamba kwa nini muuaji alifanya mauaji kwa mabilionea hao na mwisho wa siku kumuua padri ambaye kila mmoja alijua kwamba alikuwa mtu mwema, aliyewahubiria watu kuhusu maisha ya Yesu Kristo na kuwataka wote wafuate njia kuu.
FBI walichanganyikiwa, kila wakati waliita vikao, wakawasiliana na CIA na kuwaomba kufanya uchunguzi nchini Misri na Ufaransa ili kujua ni kitu gani kilitokea.
Katika sehemu hizo ambapo mauaji yalitokea, kulikuwa na majina ya wanawake wawili tofauti, nchini Misri kulikuwa na mwanaume aliyeitwa Maria Ogabugu ambaye alionekana kuwa na asili kutoka nchini Nigeria na kule Ufaransa mwanamke aliyefanya mauaji alikuwa mwanamke wa Kiislamu kwani bilionea huyo alipoingia ndani, aliongozana naye huku akiwa amevalia nikabu.
“Huyu muuaji atakuwa mwanamke! Huo ni uthibitisho wa kwanza tulioupata. Ni lazima tumtafute na tujue ni kwa namna gani tunaweza kumpata. Kitu cha kwanza kabisa ni kwenda kuzungumza na familia zao, tuwajue wanawake ambao walikuwa karibu nao, tukifanya hivyo, tutafanikiwa,” alisema ofisa mmoja wa FBI, huyo aliitwa Mark Thomson, mwanaume mwenye mwili uliojengeka ambaye kwake, kufanya upelelezi ndani ya nchi yake kilikuwa kitu kidogo na kila alipopewa kazi, ndani ya mwezi aliikamilisha.
“Basi tukaonane na familia zao!”
“Haina shida.”
Wakatumwa maofisa wawili wa kuonana na familia ya Padri Mathew huku wengine kutumwa kuonana na familia za mabilionea waliokuwa wameuawa nchini Misri na Ufaransa. Hilo halikuwa kazi kubwa, walijua kwamba kama wangezungumza na familia zao, wangepata mwanya wa kuanza kazi yao kwani mpaka kipindi hicho, hawakujua ni wapi walitakiwa kuanza, ila kwa kuwa walihisi muuaji alikuwa mwanamke, kwao, kazi ile ikaonekana kuwa ndogo kidogo.
****
Dar es Salaam, Tanzania
“Theresa! Huu ni mwaka wetu wa pili katika ndoa yetu, ungependa tufanye nini?” aliuliza mwanaume mmoja aliyeitwa kwa jina la Godfrey Kidatu, alikuwa kijana wa miaka thelathini na mbili, alikuwa na mwili uliojazia kidogo, kwenye kidevu chake kilikuwa na ndevu chache kidogo.
Alikuwa amekaa katika meza ya chakula pamoja na familia yake katika Ufukwe wa Miladiva. Mkewe, Theresa alikuwa pembeni huku wakiwa na mtoto wao aliyekuwa na miaka miwili. Kwa jinsi walivyokaa kimahaba, kila mtu aliyekuwa katika ufukwe huo uliokuwa jijini Dar es Salaam alikuwa akiwaangalia kwani walionekana kupendeza na kumvutia kila mtu.
“Tuna mengi ya kufanya ila kwanza haka katoto kaanze shule ya chekechea,” alijibu Theresa huku akimwangalia mume wake.
Godfrey Kidatu alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na maisha mazuri jijini Dar es Salaam, alikuwa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa na mafanikio makubwa katika umri mdogo.
Alikuwa kijana mcheshi, mwenye biashara nyingi zilizomuingizia kiasi kikubwa cha pesa kila siku. Maishani mwake, alikuwa na kila kitu, alikuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile kwa sababu tu alikuwa na fedha.
Alijenga jumba kubwa Masaki, alikuwa na boti mbili zilizokuwa zikifanya safari kwenda katika Visiwa vya Zanzibar, alikuwa na mabasi makubwa yaliyokuwa yakienda mikoani, kwa kifupi, maishani mwake hakuwa na shida na kila kitu alichokifanya kilimaanisha pesa.
Aliamua kutoka na mkewe kwenda katika ufukwe huo, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza ndani ya mwaka mmoja. Alitamani sana kuwa na familia yake karibu lakini kutokana na majukumu aliyokuwa nayo, hakuwa akipata nafasi hiyo hata kidogo.
Siku hiyo alipata nafasi na kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutoka na familia yake hiyo ambayo ilikuwa kila kitu. Walikaa na kuzungumza huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha tele, walitaniana na kufanya mambo mengi ya kimahaba, wakapanga mipango yao mengi, kwa kifupi, kila mmoja alitamani kumfurahisha mwenzake siku hiyo.
“Ila kuna kitu nataka kukwambia,” alisema Godfrey huku akimwangalia mke wake.
“Kitu gani?”
“Unalikumbuka lile dili la kusafirisha mchanga wa dhahabu nililokuwa nalihangaikia?” aliuliza Godfrey.
“Ndiyo!”
“Dili limetiki!”
“Unasema kweli?”
“Yeah! Nilipigiwa simu na kuambiwa kwamba nipo huru kufanya biashara hiyo na ile ya kuleta mafuta kupitia kampuni yetu mpya ya GoThe Oil Company. Nitakuwa nikileta mafuta na kuyasambaza sehemu mbalimbali hapa,” alisema Godfrey.
“Kweli?”
ITAENDELEA KESHO