
LEO tunaye mwimbaji wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Bukuku ambaye anaeleza dondoo mbalimbali juu ya mafanikio, lengo likiwa ni kumtia moyo mwanamke mwenye kiu ya kupambana na maisha.
UMT: Wengi wangependa kujua wewe ni mwenyeji wa wapi?
Bukuku: Ni mwenyeji wa Mbeya na nimezaliwa kwenye familia ya kawaida.
UMT: Nje ya uimbaji unafanya nini kingine?
Bukuku: Biashara. Ninapenda sana kujishughulisha kama ambavyo hata Biblia inaagiza kuhusu watu kufanya kazi kwa bidii ili kuepusha kuwataabisha wengine, ukisoma sana nyaraka za Mtume Paulo utagundua alikuwa mtu wa kusisitiza sana watu kufanya kazi.
UMT: Unafanya biashara gani hasa?
Bukuku: Ujasiriamali wa kilimo na mifugo, lakini pia hoteli na mambo mengine mengi ambayo yanamaanisha kukidhi mahitaji ya kila siku ya binadamu.
UMT: Ni lini ulianza kupambana na maisha?
Bukuku: Kama nilivyosema hapo awali kwamba nimezaliwa kwenye familia ya kawaida kwa hiyo kuanzia hapo ikawa na kiu ya kufika mbali zaidi na kwa kweli ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kwa hili.
UMT: Nini siri ya mafanikio?
Bukuku: Kanuni hazijawahi kubadilika. Kinachobadilishwa ni maneno na ufundi, lakini uhalisia wa nini kifanyike ili mtu afanikiwe, siri na kanuni ni zilezile (anaendelea)… Mengi yalishasemwa, lakini ninazo kanuni kubwa tatu- nidhamu, bidii ikiwa imechanganyika na malengo na dhamira ya dhati na mwisho kabisa ni kujihakikishia uhusiano bora na Mungu.
UMT: Umesema nidhamu, katika mafanikio inaingiaje? Kwa sababu ninawafahamu watu wengi sana wenye nidhamu ya hali ya juu, lakini hawajafanikiwa!
Bukuku: Nidhamu imegawanyika katika makundi matatu. Kuna nidhamu ya watu, pesa na muda. Zote ni muhimu lakini kubwa kuliko zote ni hiyo ya muda (anaendelea)… Watu wengi hujitahidi sana kuwa na nidhamu kwa watu, lakini husahau kuwa na nidhamu kwenye pesa na muda. Lazima uheshimu pesa kila inapoingia mfukoni na pesa inapoheshimika ndipo hutulia kwa mtu, lakini pia ni lazima uheshimu muda ambao ndiyo huzaa pesa na mafanikio mengine.
UMT: Wengi hujitahidi sana kufanya kazi kwa nguvu, lakini mwisho wa siku huambulia patupu, nini neno lako juu ya hili?
Bukuku: Hakuna dhambi mbaya maishani kama kukata tamaa, kosea na fanya makosa yote, lakini siyo kukata tamaa na kuruhusu mambo yaende kama yalivyo (anaendelea)… Muhimu ni kujiwekea malengo makubwa kisha kujitolea kuteseka kwa kufanya kazi kwa nguvu hadi yatimie. Fanya kazi kwa nguvu hadi viumbe wote wakiri nafsini kwamba unawajibikia maisha. Mungu hajawahi kumuacha mja wake anayehangaika na maisha na kama anayo dhamira na nia ya dhati kabisa katika kufanikiwa.
UMT: Ni mara ngapi umewahi kukutana na shuruba za maisha kwa kiwango cha kuvunjika moyo na kukata tamaa?
Bukuku: Kwanza nikusahihishe, sijawahi kukata tamaa japo nimewahi kukutana na nyakati ngumu kwa kiwango kisichotamkwa. Kipindi ambacho nyuma kuna simba, kulia kuna dubu, kushoto kuna chui na mbele kuna milima iliyozingirwa na miiba mikali ya michongoma mikavu. Maisha yanaadhibu vibaya, lakini Mungu hutuinua kwa mkono ulio mkuu.
Makala na Brighton Masalu
Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers
Android ===>Google Play
iOS ===>Apple Store