×

Okwi Ajiandae…Chirwa Apiga Hat Trick Ya Kideoni

Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa.

 

STRAIKA Obrey Chirwa amedhihirisha ubora wake baada ya jana Jumapili kuifungia Yanga mabao matatu ‘hat trick’ na kuiwezesha kushinda mabao 5-0 dhidi ya Mbeya City.

 

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Chirwa raia wa Zambia, alionyesha tangu mwanzoni kuisumbua vilivyo ngome ya Mbeya City.

 

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 20 katika nafasi ya tatu, huku Simba ikibaki kileleni mwa ligi kuu na pointi zake 22 baada ya juzi kuifunga Prisons bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

… Chirwa akifanya yake.

Azam FC ambayo jana iliifunga Njombe Mji bao 1-0, imebaki nafasi ya pili ikiwa na pointi 22 lakini inazidiwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

 

Chirwa, raia wa Zambia aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 19 akimalizia pasi ya Pius Buswita, Emmanuel Martin akafunga dakika ya 22 baada ya kupokea pasi ndefu ya Raphael Daud kisha kumpiga chenga kipa wa Mbeya City, Fikirini Bakari.

 

Hata hivyo, dakika ya 28, Martin aliifungia bao Yanga lakini mwamuzi Athuman Lazi wa Morogoro alilikataa kisha akamwonyesha kadi ya njano mfungaji kwani alitenda kosa kabla ya kufunga.

Mbeya City iliyokuwa na Mrisho Ngassa kikosini, ilijitahidi kutaka kusawazisha mabao hayo lakini ukuta wa Yanga chini ya nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ uliweza kuondosha hatari zote.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini dakika ya 49, Yanga ilipata penalti baada ya kipa wa Mbeya City, Fikirini kumchezea rafu Raphael Daud, ambapo dakika ya 50 Chirwa alifunga kwa penalty murua kabisa. Chirwa aliifungia Yanga bao la nne dakika ya 59 baada ya kuiwahi pasi ya Ibrahim Ajibu.

Leave a Comment