The House of Favourite Newspapers

Matatizo ya moyo yanavyosababisha vifo-4

NI matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wa safu hii na karibuni kujiunga nami katika makala haya maalum na tutaendelea kujadili tatizo la mshtuko wa moyo, ambalo ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kuua watu wengi duniani. Jumanne iliyopita tulisoma maelezo ya kina ya Dk. Morise Richard aliyesema kuwa mshtuko wa moyo unatokea wakati mtiririko wa damu yenye oksijeni unapozuiwa kwa ghafla katika misuli ya moyo. Iwapo mzunguko huo wa damu hautaendelea haraka, kitendo hicho huifanya
misuli ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na hivyo kuhatarisha maisha ya mtu husika.

 

FAHAMU DALILI ZA MSHTUKO WA MOYO

(Myocardial Infarction) Mshtuko wa moyo kwa lugha ya tiba unajulikana kama ‘Myocardial Infarction’ na hutokea pale mshipa mmoja wa damu au zaidi inaposhindwa kusafirisha damu yenye oksijeni katika moyo, kutokana na kuziba kwa mishipa hiyo.

 

“Mishipa ya damu inaweza kuziba kwa sababu tofauti kama vile, kuta za mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo (coronary arteries) kuwa nene, chembechembe za mafuta kujikusanya katika mishipa ya damu, kudhoofika na kukonda mishipa ya damu, mishipa ya damu inaposinjaa na kushikana au spasm na kujitokeza donge la damu katika mishipa ya damu,” anasema Dk Richard. Anafafanua:“Mshtuko wa moyo mara nyingi husababishwa na ugonjwa wa moyo wa mishipa ya damu au Coronary Heart Disease (CHD).

 

 

“Hii ni hali ambayo ndani ya mishipa ya damu hutokea kitu kiitwacho ‘plaque’ na kuzuia damu isiweze kupita katika mishipa ya damu, ambayo ni matokeo ya muda mrefu.” Lakini ni wakati gani mtu hukabiliwa na hatari ya kupata mshtuko wa moyo? Dk. Richard anasema anakabiliwa na tatizo hilo pale umri wa mtu unapoongezeka na kuwa mzee, anapokuwa na unene wa kupindukia, kuvuta sigara, kuwa na shinikizo la damu au High Blood Pressure (HBP) na kuishi bila kuwa na harakati na kutoushughulisha mwili yaani kufanya mazoezi.”

 

Mtu kuwa na kiwango cha juu cha mafuta katika damu au High Blood Cholesterol, kuwa na ugonjwa wa kisukari na kuwa na msongo wa mawazo, wasiwasi na fikra nyingi ni sababu pia. Mambo mengine yanayochangia kupata mshtuko wa moyo ni baadhi ya magonjwa ya moyo, kufanyiwa operesheni ya moyo, kuwa na ndugu katika familia ambao wana matatizo ya moyo.

 

Tunaelezwa kuwa, uvutaji sigara husababisha mshtuko wa moyo unaotokana na kuziba mishipa ya damu kwa asilimia 36, ambapo unene husababisha ugonjwa huo kwa asilimia 20. Kukaa bila kujishughulisha au kufanya mazoezi husababisha mshtuko wa moyo kwa asilimia 7-12.

 

Pia wanaume wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo zaidi kuliko wanawake katika kipindi chote cha maisha hasa kabla ya wanawake hawajafikia wakati wa kukatika hedhi. Lakini kwa ujumla kwa kuwa wanawake huishi miaka mingi kuliko wanaume, magonjwa mengine ya moyo husababisha vifo vya wanawake uzeeni zaidi kuliko wanaume. Baadhi ya wakati mshtuko wa moyo hutokea kwa dalili zilizo wazi na kwa haraka sana. Lakini mara nyingi mshtuko wa moyo hutokea polepole huku mtu akipata maumivu ya wastani na kutojisikia vyema.

 

DALILI ZA MSHTUKO WA MOYO

Mara nyingi watu wanaopatwa na hali kama hiyo huwa hawana uhakika na kile kinachotokea na husubiri kwa muda mrefu kabla ya kuomba msaada au kumuona daktari. Zifuatazo ni dalili ambazo hutokea pale mtu anapopatwa na mshtuko wa moyo. Fuatilia wiki ijayo ili uone dalili za ugonjwa wa moyo unaoweza kusababisha vifo.

Makala: ELVAN STAMBULI

Comments are closed.