
SIKU kadhaa zilizopita Watanzania upande wa Visiwani walikuwa bize wakifurahia mafanikio ya timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes ambayo ilifanikiwa kushika nafasi ya pili katika michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika nchini Kenya. Wakati michuano inaanza, Zanzibar ilionekana ni moja ya timu ‘nyanya’ ambayo ni kama wasindikizaji ambao hawatafika mbali, zaidi wataishia katika hatua ya makundi.
Upepo ukabadilika, timu hiyo ikafika fainali tena ikafungwa kwa mbinde na wenyeji wa michuano hiyo katika hatua ya penalti, hakika walistahili pongezi kwa kuwa vijana wao walifanya kazi nzuri. Kulitokea lugha kali ambayo haikuwa nzuri na ninaungana na wote waliokemea, japokuwa baadaye mashabiki w a l i o n ye s h a uungwana kwa waliomba radhi. Mara baada ya kurejea Zanzibar msafara wa timu hiyo ulipata mapokezi makubwa na baadaye kukaribishwa Ikulu kwa mwaliko maalum wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein.
Walipokuwa Ikulu Rais Shein aliwakabidhi shilingi milioni tatu kila mmoja na kuwapa viwanja, nampongeza kiongozi huyo kwa kufanya hicho alichokifanya. Zawadi ya fedha inaweza kuonekana ni ndogo lakini ina umuhimu mkubwa katika medani ya soka kwa kuwa inawapa moyo wachezaji wengine kuwa siku wakitumikia vema taifa lao basi nchi itawafikiria na kuwaonyesha thamani yao. Zawadi ya kiwanja hii ndiyo kubwa kuliko, kwani itadumu miaka zaidi ya 50 na yawezekana hadi hiki kizazi cha wachezaji hao kinapotea kwenye ulimwengu thamani ya viwanja walivyopewa ikaendelea kuwa kubwa kila mwaka.
Narudia tena kuipongeza Serikali ya Zanzibar kwa maamuzi waliyoyafanya kwa wachezaji na benchi lao la ufundi, baada ya hapo kuna mambo kadhaa ambayo ni vema niyazungumze hasa kwa kuwa yamezungumzwa na Dk Shein. Katika hotuba yake ya kuwakabidhi zawadi hizo, alisema hataki kusikia wameuza viwanja hivyo na kuwaonya
kuhusu migogoro ya viongozi kiasi cha kufikia kupelekana mahakama za kiraia.
Soka ina taratibu zake na ndiyo maana kesi zao huwa zinapelekewa kwenye mamlaka yao, alichosema rais kinamaanisha kuna watu huwa wanataka kujiona wao ni wakubwa kuliko mamlaka za soka kitu ambacho mwisho wake kinaweza kuiharibia Zanzibar na kupata hasara kubwa. Moja ya tatizo kubwa la kutoendelea kwa soka la Zanzibar licha ya vipaji vingi vilivyopo ni kukosa uongozi bora, wengi waliopo wanatanguliza migogoro zaidi kuliko kufanya kazi za maendeleo. Miezi ya hivi karibuni walionekana angalau kutulia na kuwa wamoja, mwisho wa hicho kilichotokea ni kuwa tumeona mafanikio ya Zanzibar Heroes, lakini hapo nyuma ilikuwa ni nadra kupita miezi mitatu au sita bila kusikia kuna mgogoro iwe ni ngazi ya wilaya, mkoa au taifa.
Nimwambie Rais Shein kuwa Zanzibar kuna vipaji vingi lakini sumu kubwa ni kwenye uongozi. Wachezaji hawawezi kucheza na kujisimamia wakati huohuo, kila mtu akifanya majukumu yake ni rahisi kupiga hatua. Upepo kama huo ndiyo uliokuwepo katika uongozi wa soka wa miaka kadhaa uliopita upande wa Bara enzi za FAT, hata uongozi uliopita kulikuwa na matatizo ya hapa na pale lakini hayakuhusisha migogoro baina ya viongozi wao kwa wao kama inavyotokea Zanzibar mara kadhaa. Alipokuwa akihutubia, Rais Shein alisisitiza juu ya kutouza viwanja hivyo, niliwaza mara kadhaa sababu ya kiongozi huyo kutoa msisitizo huo, nikajua yawezekana anajua mazingira ya ‘vijana’ wake au wale wanaowazunguka.
Kwa mantiki hiyo, alichokifanya Dr Shein ni deni kubwa wa wanasoka wa Zanzibar kuanzia wachezaji, viongozi hadi wadau ambao ni mashabiki, wadhamini na makampuni mbalimbali yanayowekeza katika mchezo huo. Huu ni muda wa viongozi wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kutafakari hotuba hiyo na kujua nini cha kufanya ili kuondoa wingu zito lililo mbele yao kukuza mchezo wa soka, hamuhitaji kuzungumza kwenye vyombo vya habari bali majibu yenu yawe kwa vitendo.
STORI NA JOHN JOSEPH