
NI matumaini yangu mpenzi msomaji umesherehekea vyema Sikukuu ya Krismasi kwa amani na utulivu, kikubwa ni uzima na afya njema tukisubiri mwaka mpya wa 2018. Kwanza kabisa nitoe pole zangu kwa mashabiki wa Simba ambao Ijumaa iliyopita walikumbana na kadhia kubwa baada ya kuvuliwa ubingwa kwenye michuano ya Kombe la FA katika mchezo wao wa awali kabisa dhidi ya Green Warriors.
Kitendo cha Simba kuondolewa kwenye michuano hiyo, kimewaumiza mashabiki wao wengi kutokana na mategemeo yao ambayo waliweka kwa wachezaji wao na benchi la ufundihuku wengi wakiamini kuwa timu hiyo ingefika mbali kwenye michuano hiyo.
Lakini matokeo ya kuondolewa na timu ya Green Warriors inayoshiriki Ligi Daraja la Pili kwa penalti 4-3 baada ya muda wa kawaida kutoka sare ya bao 1-1, hayakumuacha salama kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog kwani safari yake iliishia hapo baada ya uongozi kutoridhishwa na mwenendo wake.
Ni wazi na inafahamika kuwa Simba ina wachezaji wazuri na wenye uwezo na bado imesajili wengine lakini uwezo wao uwanjani umekuwa sio mzuri jambo ambalo linawakatisha tamaa mashabiki wao hata wengine kuugua presha kutokana na kiwango kibovu ambacho wanaonyesha tofauti na matumaini yao.
Tunafahamu kwenye soka hakuna timu ya kudharau lakini swali kwa Simba ambayo imesheheni wachezaji wenye uwezo mkubwa walishindwa kujipanga au waliwadharau Green Warriors kuwa ni timu ya chini kwamba lazima watashinda tu! Hilo jibu wanalo wenyewe. Hili la Simba halina tofauti kabisa na lile la Manchester United katika Kombe la Carabao ambapo hivi karibuni waliweza kutolewa hatua ya robo fainali na timu ndogo tu Bristol City na hii ni kutokana na kuidharau tu lakini mwisho wa siku iliweza kuwagharimu.
Safari ya Simba kwenye michuano hiyo imekomea hapo ingawa tayari wana tiketi ya msimu uliopita kushiriki michuano ya kimataifa na wao watashiriki Kombe la Shirikisho na kwa sasa wasipopambana kwenye Ligi Kuu Bara hiyo itakula kwao kwa sababu ndiyo tiketi pekee ya wao kujihakikishia kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/19.
Inaumiza kwa kiasi kikubwa hasa kwa mashabiki pamoja na wadau ambao wamekuwa wakijitoa kwenye klabu hiyo kuhakikisha inafanya vizuri kwa kujinyima kwao lakini mwisho wa siku mambo yanakuwa tofauti kwao. Lakini hata hili la kocha kutimuliwa siyo tiba mbadala kwamba timu ita
fanya vizuri kwa sababu si mara ya kwanza Simba kutimua kocha wake, huenda kuna madudu mengine tofauti na hili hivyo viongozi wanapaswa kuliangalia hilo.
Simba inatakiwa kujiangalia upya uwezo wake na mipango yake kama wakishindwa kujipanga wataishia kufukuza makocha tu bila kujua tatizo liko wapi. Leo hii Omog ameondoka atakuja mwingine lakini huenda tatizo likawa lilelile kama uongozi hautafanya uchunguzi zaidi. Wachezaji wajipange pia watafakari na kukumbuka kuwa wao ndiyo chachu ya mafanikio ya klabu, wanapaswa kutambua kuwa kuna watu kibao mnawaumiza pale mnapofanya vibaya, simameni na pambaneni ili muwape raha mashabiki wenu ambao wamekuwa wakilipa viingilio kila mnapocheza mechi zenu.
Kutolewa kwenye FA isiwe mwisho wa safari yenu, kumbukeni mna michezo ya ligi kuna, Shirikisho Afrika na Kombe la Mapinduzi hivyo mkiamua kupambana hapo basi mtaandika historia ya kipekee kikubwa msikate tamaa kwani kila kazi ina changamoto zake. Angalieni wapi mlikosea na huu usiwe muda wa kutafuta mchawi ni nani zaidi muangalie nini kipo mbele yenu, Simba ni timu kubwa mashabiki wanataka mafanikio wanatamani kupata ubingwa wa ligi kuu kwani wameumisi kutokana na mpaka sasa kupita zaidi ya misimu minne bila taji hilo.
STORI NA MARTHA MBOMA