
BARCELONA, Hispania
MSIMU uliopita Barcelona ilikuwa nyanya, haikuweza kufurukuta mbele ya Real Madrid lakini msimu huu hadi sasa katika Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ wao ndiyo wanaongoza kwa pointi 51.
Madrid ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 32 wakati Atletico Madrid ni ya pili na pointi 42 halafu Valencia ni ya tatu na pointi 40. Barcelona ina mabao 52 na imeruhusu mabao tisa tu katika wavu wake.
Jumapili iliyopita, Barcelona ilitoka nyuma ikiwa imefungwa mabao mawili na kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Real Sociedad kwenye Uwanja wa Anoeta.

Kabla ya mechi ya Jumatano wiki hii ya Copa del Rey ambapo Barcelona ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Espanyol, timu hiyo ilikuwa imecheza mechi 29 msimu huu katika michuano yote bila kupoteza hata mechi moja.
– Mechi 39: 32W 7D (Lucho 2015-16)
– Mechi 29: 23W 6D (Valverde 2017-18)
– Mechi 28: 23W 5D (Guardiola 2010-11)
Hapa chini ni mambo yanayoifanya Barcelona ifanye vizuri msimu huu;
#5 Mbinu za Valverde ni bomba
Baada ya kuaminiwa na kupewa kazi ya kuinoa Barcelona mwaka jana katikati, Ernesto Valverde ameonyesha chaguo lake limeonekana kuwa sahihi na ameonyesha kweli kazi anaiweza.

Kwa msimu huu, Valverde ameamua kubaki katika mfumo wa 4-4-2, tofauti na ule wa 4-3-3 au 3-4-3 uliokuwa ukitumiwa na Luis Enrique misimu iliyopita. Valverde ni muumini wa usawa na kucheza soka la shoka na hapendi kuruhusu udhaifu wowote kwa adui.
Katika mfumo wake, mabeki wa pembeni wanacheza kwa kushirikiana vizuri na viungo wa kati hivyo kuongeza nguvu ya kujilinda na kushambulia kwa wakati mmoja.
Usajili mpya wa Paulinho, umeweza kusaidia kuweka daraja imara kati ya viungo na washambuliaji ambao ni Lionel Messi na Luis Suarez.

#4 Hana majeruhi wengi
Wachezaji 17 wa Barcelona ambao wanaweza kuingia kikosi cha kwanza muda wowote, wote ni wazima na hawajaandamwa na majeraha msimu huu. Lakini ni wanne tu ambao ni majeruhi hao ni Samuel Umtiti, Ousmane Dembele, Andre Gomes na Arda Turan. Hawa wapo nje ya uwanja kwa wiki kadhaa hadi watakaporejea uwanjani.
Hali ni tofauti kwa Real Madrid, ambayo ina wachezaji sita ambao wapo nje ya uwanja kwa wiki tatu na wengine hawawezi kucheza tena msimu huu, majeruhi ni tatizo kwa timu yao.
Karim Benzema na Gareth Bale wameshaumia mara mbili mpaka tatu na kukaa nje kwa wiki kadhaa ndani ya msimu huu tu, hivyo timu kukosa mchango wao.
Barcelona yenyewe mtu kama Messi ambaye ni muhimu kwao, wala hajaumia kiasi cha kuwa nje ya uwanja na ndiyo kwanza anazidi kufanya vizuri.
#3 Kujiamini kutoka taabani
Katika Supercopa mwaka jana walipigwa mabao 5-1 na Madrid halafu mwezi huohuo wa Agosti mchezaji wao Neymar akaondoka kwenda Barcelona, haya ni mapigo mawili yaliyoikumba Barcelona mwaka jana.
Ajabu ni kwamba, licha ya mapigo hayo, Barcelona ilitulia na kujipanga na unaweza kusema imekuwa kama hamasa kwao ya kuwa imara na wapambanaji wa muda wote uwanjani.
Timu ikajipanga na kufanya vizuri ambapo hadi ikacheza mechi 29 bila kufungwa huku wachezaji wake wakicheza kwa kujiamini muda wote.
#2 Beki ya nguvu
Ernesto Valverde amejitahidi kutengeneza ukuta wa Berlin katika safu yake ya ulinzi katika kikosi cha Barcelona. Katika mechi 31 walizocheza chini ya kocha huyu, Barcelona haijaruhusu bao katika mechi 20, zikiwemo 12 za La Liga.
Wamefungwa mabao tisa tu katika La Liga msimu huu, wamezidiwa na Atletico Madrid tu ambao wameruhusu mabao nane tu. Barcelona ina tofauti ya mabao ya 43. Katika vinara wa ligi tano bora Ulaya, Barcelona inaongoza kwa kuruhusu mabao machache zaidi.
Uwepo wa Yerry Mina na Nelson Semedo pia Umtiti unaifanya safu ya ulinzi ya Barcelona kuwa imara na yenye kupambana muda wote.
#1 Lionel Messi
Msimu huu, Messi ameonyesha yeye ni mtu muhimu katika kikosi cha Barcelona akionyesha uwezo wa hali ya juu akionyesha nia hasa ya kuisaidia timu yake kufikia malengo yake na anaibeba timu.
Messi msimu huu amekuwa hodari katika kufunga mabao, kutoa pasi za mwisho yaani asisti na kuongeza umoja kikosini kwa nia ya kupata ushindi wakati wote.
Katika mechi 28 alizoichezea Barcelona msimu huu, Messi amefunga mabao 23 yakiwemo 17 aliyofunga katika La Liga huku akitoa asisti 11 katika michuano yote.
Kama Messi akiendelea kufanya vizuri katika kikosi chake msimu huu, ni wazi kuwa Barcelona itapata mataji mengi kwani hata mpinzani wake Madrid hana kiwango cha kutisha.