The House of Favourite Newspapers

Serikali Kumshughulikia Nabii Tito

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba amesema hamtambui mtu anayejiita nabii Tito na kwamba hajasajili kanisa lake katika ofisi ya msajili wa taasisi za dini.

Komba amesema Serikali imeona vitendo anavyovifanya ‘nabii’ huyo kupitia mitandao ya kijamii na imeanza kuchukua hatua.

“Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna mtu anayezuiwa kuongea hapa nchini, mwache aongee anavyoweza ila Serikali imeshaona anachokifanya na yanayoendelea mitandaoni hatua zinachukuliwa dhidi yake,” amesema Komba.

Kauli hii imekuja kufuatia kusambaa kwa video mbalimbali zikimuonyesha ‘nabii’ huyo akitoa mafundisho yake huku akinywa vilevi pamoja na kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maadili ya dini, jambo ambalo limeonekana kuwakera wadau wengi wa dini.

Kwa upande wao viongozi mbalimbali wa dini wameonyeshwa kukerwa na kulaani vitendo anavyovifanya mtu
huyo anayejiita ‘nabii’ na kusisitiza kuwa hakuna dini inayoruhusu hayo.

Askofu Msaidizi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza amesema kuwa, kutokana na vitendo anavyofanya, mtu huyo hapaswi kujiita mtumishi wa Mungu.

“Huyo hawezi kuwa mtumishi wa Mungu na wala hafanyi huduma ya kanisa. Ni vyema watu kama hawa wafuatiliwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Natumaini Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ndani yake ina ofisi ya msajili wa taasisi za dini itafanya kazi yake,” amesema Mchungaji Lwiza.

Naye Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajab Katimba amesisitiza Serikali na viongozi wa dini kuingilia kati suala hilo na kueleza kuwa, hakuna kitabu chochote cha dini kinachohamasisha ulevi na ukosefu wa maadili.

“Hilo suala linakwenda tofauti na dini na mila na desturi zetu pia. Dini zinatakiwa kuleta amani na kuhamasisha watu waheshimiane si kuzungumza mambo yanayokiuka maadili yetu. Naona ipo haja ya viongozi wa dini na Serikali kuingilia suala hili na waende mbali zaidi kwa kuongea naye huenda hafahamu anachokifanya,” amesema Rajab Katimba.

Comments are closed.