
AMA kweli kuna watu hawana huruma! Wakati staa wa filamu Bongo, Wastara Juma akihangaika kutafuta msaada wa shilingi milioni 37 kwa ajili ya matibabu ya mguu wake unaomsumbua kwa muda mrefu, baadhi ya watu wasiojulikana wanadaiwa kucheza mchezo mchafu wa kuzipiga juu kwa juu fedha zake ambazo zimekuwa zikitumwa kupitia simu yake ya mkononi.
Chanzo chetu kulicho karibu na Wastara kilimweleza mwandishi wetu kuwa, tangu ameanza kuchangiwa baada ya kujitangaza gazetini na kwenye vyombo vingine vya habari, kuna watu wengi ambao wamemwambia wamemtumia pesa, lakini kwenye simu yake hazionekani.
“Yaani kwa kweli Wastara anatia huruma, inavyoonekana kuna watu ambao wanamhujumu kwa kuzichukua pesa zake ambazo zimekuwa zikitumwa kupitia namba yake ya Tigo, hajui ni mchezo gani unafanyika, lakini inavyoonekana ni mamilioni ya pesa yameshapigwa na wajanja, ana mpango wa kwenda kufuatilia kule Tigo,” alidai mtoa habari huyo aliyeomba hifadhi ya jina.
Waziri Mwakyembe akimpa pole Wastara.
RISASI KWA WASTARA
Katika kujua kinachoendelea kwenye ukusanyaji wa pesa zake za matibabu, mwandishi wetu alifunga safari hadi nyumbani kwa Wastara, Tabata jijini Dar ambapo alipopatikana alifungukia wizi anaohisi unafanywa na watu wasiojulikana.
“Inavyoonekana kuna pesa zangu nyingi sana zimepigwa. Baada ya kujitangaza kuomba msaada, kuna kipindi hapo katikati pesa ziliingia sana kisha zikakata. Nilikaa kwa takriban siku 9 hela haziingii, watu wakawa wananipigia simu na kuniambia kuwa, wametuma pesa. Nilipoenda pale Tigo wakaniambia kuna ‘jam’ kubwa sana na pesa wakiziangalia kule wanaziona nyingi tu, lakini kwenye laini yangu hazionekani.
“Ilibidi niombe wanisaidie ili niweze kupata pesa zangu na wakaniambia niende Jumatatu (juzi). Lakini Tigo waliniambia kuwa, laini yangu kwa siku kiwango cha juu natakiwa nipokee milioni tatu na mara ya mwisho kuangalia kulikuwa na laki mbili na nusu tu, kwa hiyo hapo kuna kitu, ngoja nione Tigo watanisaidiaje,” alisema Wastara.

MADAI YANAYOMSIKITISHA
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko juzi, Wastara alionesha kusikitishwa na maneno ya baadhi ya wasanii wenzake ambao wanamuona kama anautumia mguu wake katika kujipatia pesa wakati ukweli hauko hivyo.
“Wapo wanaosema eti nimegeuza mguu wangu mtaji, jamani hivi naweza kufanya kitu hicho kweli? Hivi hawaoni ninavyoteseka na huu mguu? Inaniuma sana,” alisema Wastara na kuongeza:
“Mtakumbuka huu mguu haujaanza kunisumbua leo. Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na wasamaria wema wengine walinisaidia sana. Hivi ninawezaje kutumia usanii wa kujiingizia pesa kwa mguu wangu huu kisha viongozi wakuu wa nchi nikawahusisha? Mungu ndiye anajua.
“Kikubwa niwashukuru tu wale ambao mpaka sasa wamenichangia. Namshukuru sana Waziri Mwakyembe, Mama Samia, Ali Kiba na Watanzania wengine ambao siwezi kuwataja. Wale ambao bado wana nia ya kunichangia, wafanye hivyo na Mungu atawalipia. Nilikuwa natafuta milioni 37 na mpaka sasa zimebaki milioni 17 kufikia lengo. Nimeshaanza utaratibu wa kwenda kufanya matibabu kwa mwezi ujao.”
STORI: Hamida Hassan, Risasi Mchanganyiko