×

REKODI YA DJUMA YAMTISHA MFARANSA SIMBA

Kocha Pierre Lechantre.

 

KOCHA wa Simba, Pierre Lechantre amewadokeza viongozi kwamba amezikubali rekodi za Mrundi, Masoud Djuma na akishirikiana nae watapiga mzigo kwa kwenda mbele.

Djuma alijiunga na Simba hivi karibuni kama kocha msaidizi lakini baada ya kutim­uliwa kwa aliyekuwa Kocha wa Simba, Joseph Omog, kocha huyo alipewa nafasi ya kuwa kaimu kocha mkuu ndani ya kikosi hicho kazi ambayo amei­fanya vyema.

Pamoja na kocha huyo kushindwa kufanya vizuri kwenye Kombe la Mapinduzi, lakini ameonyesha kuwa na ubora wa hali ya juu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Djuma baada ya kuachiwa timu hiyo, ameiongoza kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo yote ameibuka na ushindi.

Kocha huyo alianza akiwa bosi kwenye mchezo dhidi ya Ndanda ya Mtwara wakiwa ugenini ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Baada ya mchezo huo, Djuma aliiongoza tena Simba kwenye mchezo dhidi ya Singida United, ambao ulitajwa kuwa mgumu kwa timu hiyo lakini akaonyesha ubora wake kwa kushinda mabao 4-0. Kichapo hicho ni kikubwa tangu kuanza kwa msimu huu wanakipata Singida United.

Mchezo wa tatu wa Djuma katika ligi ulikuwa ugenini tena ambapo timu yake ilivaana na Kagera Sugar na kuibuka na ushindi mzuri wa mabao 2-0.

Mfaransa alivyoanza kuinoa Simba.

Hii inaonyesha kuwa Djuma ana uwezo mzuri wa kuipanga timu hiyo ambayo katika michezo mitatu haijafungwa bao lolote, huku yenyewe ikiwa imepachika mabao nane. Huko nyuma kwenye michezo 10 timu hiyo ilikuwa imefunga mabao 19.

Katika michezo hiyo, mshambuliaji wa Simba John Bocco ndiye kinara kwake aki­wa amefunga mabao matatu, Emmanuel Okwi mawili na mengine yamefungwa na Shiza Kichuya, Asante Kwasi na Said Ndemla.

Hii inamaanisha kuwa kama ikitokea Mfaransa akitaka kuondoka kwenye kikosi cha Simba, basi Mrundi Masoud anaweza kufanya kazi nzuri.

Kocha pekee mzalendo mwenye heshima kubwa ndani ya Simba, Abdallah Kibadeni alisema; “Ameanza kwa rekodi nzuri, kitu ambacho nimekiona ni kwamba kuna wachezaji ambao Omog alikuwa hawatu­mii, huyu Djuma anawatumia na ndiyo wanaleta matokeo mazuri.”

Kocha Djuma mwenye jezi nyeupe.

IMEANZA LEO BANDARI

Lechantre na msaidizi wake Aimen Mohammed Habib raia wa Tunisia leo jioni wameaanza kibarua chao kwa kufanya kikao kizito na wachezaji.

Mfaransa huyo ambaye hadi jana Jumanne jioni kibali chake cha kazi kilikuwa hakijaka­milika, uongozi umesisitiza kwamba ataanza kazi leo na mambo yote yatakuwa sawa.

Bosi huyo mwenye rekodi kubwa kuliko kocha yoyote aliyewahi kufundisha nchini, alitua Jumatano na kusaini mkataba mfupi na viongozi wakasisitiza kuwa mechi yake ya kwanza itakuwa dhidi ya Majimaji FC katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kocha huyo, anatua kuifundisha Simba akirithi mikoba ya Mcameroon, Joseph Omog aliyesitishiwa mkataba wake baada ya vion­gozi wa juu kujiridhisha kuwa maji yamezidi unga.

 

Mwandishi wetu, Dar es Salaam