
IKIWA ni kikao cha kwanza cha mkutano wa 10 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ally Salehe amesusa kusoma maoni ya upinzani ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kukataa kusomwa kwa baadhi ya maneno yaliyomo katika maoni hayo.
Katika tukio hilo, Salehe alikuwa akisoma maoni hayo leo Januari 30 mwaka 2018 kwa niaba ya msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi Novemba 7 mwaka jana.
Maneno yaliyozuiwa na Chenge kusomwa na upinzani ni kuhusu matukio ya uhalifu nchini, likiwemo la kushambuliwa kwa Lissu ambapo Salehe alianza kusoma maneno hayo lakini alipofika aya ya nne alikatizwa na Chenge akimtaka asubiri, na baadaye kumueleza kuwa lugha iliyotumika katika ukurasa kwa kwanza na pili wa hotuba hiyo si ya Kibunge.
Salehe ameeeleza kuwa upinzani unaiamini na unaisimamia hotuba hiyo kwa kuwa wabunge wote wanayo nakala yake, akaomba kuiwasilisha na kurejea kuketi.