Yondani Awashangaza Yanga
BEKI wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, juzi Jumamosi alifanya jambo ambalo liliwaacha vinywa wazi wapenzi na mashabiki wa timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Lipuli FC kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.
Katika mchezo ambao Yanga ilishinda mabao 2-0, Yondani hakutakiwa kucheza kutokana na kuwa mgonjwa kama ilivyokuwa kwa Andrew Vincent ‘Dante’.
Waliotakiwa kuiongoza safu ya ulinzi ya Yanga katika mechi hiyo ni Juma Makapu na Maka Edward, lakini baada ya Yondani kuona hivyo aliamua kujitoa na kumwambia kocha wake mkuu, Mzambia, George Lwandamina kuwa itabidi acheze kwa ajili ya kuisaidia timu yake ili iweze kupata ushindi.
Akizungumza na Championi Jumatatu, mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Yanga ambaye aliomba kutotajwa jina lake akihofia kuchukuliwa hatua kwa sababu ametoa siri ya timu kinyume na taratibu, alisema kuwa mwanzoni Lwandamina alikataa Yondani asicheze lakini baada ya kushauriana na wenzake aliamua kumpanga.
“Hakika jamaa ameonyesha kuwa ni mchezaji wa aina gani ambaye yupo tayari kuhatarisha maisha yake kwa sababu ya timu.
“Kwa kiwango alichoonyesha katika mechi hii licha ya kuwa anaumwa, alimshangaza pia Lwandamina,” alisema kiongozi huyo.
Alipoulizwa Yondani kuhusiana na hilo hakuwa tayari kusema chochote lakini Lwandamina alisema kuwa anampongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya katika mechi hiyo japokuwa hakuwa fiti kwa asilimia miamoja.
Sweetbert Lukonge, aliyekuwa Iringa
Comments are closed.