
Wanafunzi ambao alikuwa akisoma nao marehemu Chuo cha NIT wakiwa msibani hapo. Wa kwanza kushoto ni mshauri wa wanafunzi, Paulina Tarazo, Agripina Joseph, Beatrice Charles na Komba Anthony wakiwawakilisha wenzao.
MWILI wa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwilini umewasili nyumbani kwao Rombo-Mashati mkoani Kilimanjaro leo Alhamisi, Feb. 23, 2018 majira ya saa 1: 45 asubuhi kwa ajili ya mazishi.

Akiongoza msafara wa waombolezaji waliopeleka mwili huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo na Mkuu wa Chuo cha NIT, Prof. Zakaria Mganilwa wamekabidhi mwili huo kwa familia.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, shughuli ya kuaga mwili wa marehemu itaanza saa 5:00 asubuhi ambapo mwili utapelekwa kanisani kwa ajili ya ibada ya kuagwa na mazishi yatafuata.

Aidha, kwa sasa wanaosubiriwa ili kuendelea na shughuli hiyo ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na viongozi wengine.

Akwilina aliagwa jana Alhamisi katika viwanja vya NIT vilivyopo Mabibo, Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda kijini kwao.





