The House of Favourite Newspapers

Baba: Nikifa Dimpoz Asinizike!

Ommy Dimpoz.

Ni kama wanaigiliziana kwani baada ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumtelekeza baba yake, Mzee Abdul Jumaa ingawa kwa sasa wako vizuri, msanii mwenzake, Omary Faraji Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ naye ameingia kwenye mkumbo huo baada ya baba yake mzazi, Faraji Nyembo kuibuka na kusema hata akifa asimzike, Risasi Mchanganyiko limeelezwa.

Msingi wa madai ya baba Dimpoz ni kwamba mwanaye huyo hamjali na hajawahi kumjali kwa chochote kabla na hata baada ya kuwa staa.

Baba Dimpoz akiongea na simu.

BATA LA DIMPOZ HUKO IBIZA

Kabla ya baba Dimpoz kufunguka ya moyoni, uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, licha ya Dimpoz kujiachia kwa kula bata sehemu maarufu za starehe duniani kama Ibiza nchini Hispania akiwa na Mwanasoka wa Uingereza, Wayne Rooney, baba yake anaishi mkoani Tabora katika lindi la umaskini, jambo ambalo linawashangaza wanaoishi karibu naye.

“Hivi mna habari kwamba baba mzazi wa Dimpoz ana maisha magumu sana huku Tabora? Kwa taarifa yenu huyu mzee anaishi kwa kubangaiza kwenye Bajaj tofauti na jina alilonalo mwanaye Dimpoz kwani ana jina kubwa ambalo ana uwezo wa kumsaidia baba yake, akawa anaishi maisha mazuri yenye hadhi kuliko alivyo sasa.

“Ngoja niwatumie picha za baba Dimpoz akiwa mtaani, akila mihogo na kachumbari kwa mamalishe maana ndiyo maisha yake, si unajua maisha ya sasa wakati mwingine hata hiyo Bajaj hailipi maana anaweza kukaa hata siku nzima hajapata mteja na huku mkoani mambo ni magumu sana,” alieleza mmoja wa marafiki wa mzee huyo.

RISASI LAINGIA MZIGONI

Baada ya kupata habari hizo kwa kina, Risasi Mchanganyiko lilifanya jitihada za kumpata baba wa Dimpoz na kufanikiwa kuzungumza naye ambapo alieleza kwamba hawezi kumlaumu sana mwanaye ila anatakiwa ajue wajibu wake kwa mzazi.

Alisema kuwa, anachojivunia ni kwamba ameshamleta Dimpoz duniani maana hakuna kitu kikubwa kama kuletwa duniani kwani asingemleta, basi hakungekuwa na mtu anayeitwa Omary Nyembo.

“Hakuna kitu kikubwa duniani kama kuletwa duniani…hayo mengine ya kwamba alilelewa na upande mmoja tu wa mama, ni madogo tu hivyo sina kosa kwa kuwa nilishamleta duniani na ninamshukuru Mungu ananipa nguvu ya kufanya kazi kwani nina Bajaj yangu niliyonunua mwenyewe ninapambana na maisha, nina umri wa miaka 64, lakini bado ninapambana.

AMTAJA WEMA SEPETU

“Ni kama Wema Sepetu anavyohangaika kutafuta mtoto, siku akimpata hata kama hamsaidii chochote atamshukuru tu Mungu hivyo na mimi huwa ninamshukuru Mungu maana nimeshamleta Omary duniani.

“Yeye kama mtoto, ndiye anayetakiwa kujua mzazi wake anahitaji nini, yaani ukimuuliza sasa hivi Dimpoz akupe namba yangu, utaona, atakujibu nini maana ninaamini hana. Nimekuwa nikimpigia, lakini simu yake unaambiwa inatumika, angekuwa anaona umuhimu si angekuwa na namba maalum kwa ajili ya kuwasiliana na mimi baba yake kama mastaa wengine wanavyofanya kuwa na namba kwa ajili ya mashabiki na nyingine ya watu muhimu,” alisema baba huyo.

Dimpoz na Wema.

NIKIFA ASINIZIKE

Baba Dimpoz hakuishia hapo kwani aliendelea kutiririka kuwa, ikitokea siku ameaga dunia na Dimpoz akatangaza au kwenda Tabora kwa ajili ya msiba, watu watamkimbiza kwa kuwa hana ushirikiano nao na wanaona maisha anayoishi watamshushia kipigo cha aina yake.

“Mfano nikifa kama leo ni bora huyo Ommy asinizike au kuja Tabora maana watu watampiga na kwanza atasema ni nani wake amefariki dunia maana hivi niko hai hana ushikiano,” alisema baba huyo.

 

DIMPOZ ANASEMAJE?

Ili kuujua ukweli, naye anazungumziaje suala hilo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Dimpoz ambapo simu yake iliita bila kupokelewa na alipotumiwa meseji kwa njia ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp na kuelezwa madai hayo yote kinagaubaga alijibu kwa kifupi: “Nipo hospitalini.”

Alipoulizwa kama anaumwa au anafanya nini hospitalini, hakujibu na hata alipotakiwa kwenda kwenye hoja ya msingi juu ya madai ya baba yake, pia hakujibu.

 

MASTAA WENGINE

Dimpoz anapita kulekule alikopita Diamond na baba yake hivyo gazeti hili linamtaka kuyamaliza mambo hayo na mzazi wake huyo kwani manung’uniko ya wazazi huondoa kabisa baraka kwenye maisha ya mtoto.

 

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko

Imeandikwa na Gladness Mallya na Sifael Paul.

Comments are closed.