
MWANASIASA wa upinzani Kenya aliyeidhinisha kiapo cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa ‘Rais wa Wananchi’ Januari Miguna Miguna ametimuliwa tena kutoka nchini humo. Mwanasiasa huyo ametimuliwa huku mzozo kuhusu uraia wake ukiendelea.
Bw. Miguna ameandika kwenye Facebook kwamba ameamka na kujikuta yuko Dubai na kwamba anahitaji matibabu. Amesema anafahamu kwamba kuna mpango wa kumpeleka London lakini anataka kupanda ndege ya kurejea Nairobi pekee.
Mwanasiasa huyo amesema amesindikizwa na ofisa wa idara ya ujasusi.
Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.
Mawakili wa Miguna wamethibitisha kwamba aliondolewa nchini humo kwa kutumia ndege ya shirika la Emirates iliyokuwa inaelekea Dubai.