×

Pretty Aeleza Alivyokesha Akilia, Kisa Waziri

Suzan Michael ‘Pretty Kind’ akiwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza

 

BAADA ya kusamehewa na kuruhusiwa kuendelea na sanaa, msanii wa muziki na filamu za Kibongo, Suzan Michael ‘Pretty Kind’ amefunguka jinsi alivyokesha baada ya kupata wito kutoka kwa waziri wa kufika katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

 

Akizungumza na Za Motomoto News, Pretty alisema kuwa, siku aliyopigiwa simu na katibu wa wizara hiyo na kumweleza kwamba anatakiwa kufika wizarani hapo kwa kuwa anahitajika na Waziri Dk Harrison Mwakyembe alijikuta akikesha usiku mzima, akiwaza ni kitu gani anachoitiwa.

 

“Sikulala hata lepe la usingizi maana nilikuwa na wasiwasi, huenda nina msala mwingine au vipi, sitasahau nilivyohaha, kulipokucha nikaenda ndiyo nikapewa taarifa njema kwamba nimesamehewa, hii ni baada ya kuandika barua kama tatu za kuomba msamaha na nashukuru kwa kuwa ombi langu kujibiwa,” alisema Pretty.

 

Januari, mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alimfungia Pretty kufanya sanaa kwa muda wa miezi sita kufuatia tabia yake ya kutupia picha mtandaoni akiwa nusu utupu na kwenye video ya wimbo wake, lakini adhabu hiyo imetenguliwa hivi karibuni baada ya msanii huyo kuomba radhi na sasa ameruhusiwa kufanya sanaa kama kawaida.