×

Mama Awekwa Mahabusu na Mwanaye wa Miezi 6, Mtoto Afariki! – Video

Ashura Theodenest akisimulia.

SAKATA la kifo cha mtoto mchanga wa miezi sita, Halfani Lema, mkazi wa Ibanda Kata ya Nyegezi jijini Mwanza, limechukua sura mpya baada ya mama yake mzazi aliyewekwa naye mahabusu, Ashura Theodenest (26), kulieleza Ijumaa Wikienda undani wa tukio hilo.

 

Madai mazito ni kwamba, mtoto huyo alifariki dunia saa chache baada ya mama yake kuachiwa kutoka Kituo cha Polisi cha Igogo, Nyegezi hivi karibuni alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za wizi wa simu ya mkononi.

Mwili ukiswaliwa kabla ya kuzikwa.

SIMULIZI YA KUKUTOA MACHOZI

Mara baada ya kujiri kwa tukio hilo, Ijumaa Wikienda lilifika maeneo hayo na kuzungumza na mama huyo ambapo alisimulia:

“Nilikamatwa kwa kusingiziwa kuwa nimeiba simu ya jirani yangu.

“Polisi waliniweka kituoni kwa siku mbili nikiwa na mwanangu wa miezi sita.

“Nilikuwa nikiwalalamikia mara kwa mara kuwa mwanangu niliingia naye akiwa mzima kabisa, lakini baada ya kukaa naye ndani hali yake ilianza kuwa mbaya.

“Nilipoona hali ya mwanangu inazidi kuwa mbaya, niliwaomba nijidhamini mwenywe, lakini walinikatalia.

“Hali ya mwanangu ilianza kubadilika, mtoto alianza kuishiwa nguvu.

“Niliwaomba polisi msaada waniruhusu nimpeleke mwanangu hospitalini, lakini walikataa.

“Waliniambia ‘kama huna mdhamini sisi cha kukusaidia hatuna na aliyekushtaki hajaja, tumsubiri yeye ili achukue uamuzi’.

Mashuhuda.

“Niliendelea kuwasihi polisi kuwa sina ndugu wa karibu wa kunidhamini hivyo wawe wema wanisaidie kuokoa maisha ya mwanangu, lakini walikataa.

“Mwanangu aliendelea kuzidiwa hadi akawa anashindwa kupumua kabisa.

“Kila polisi aliyekuwa anakuja alikuwa anashtuka kuniona nipo lokapu na mtoto mchanga, kila mmoja aliogopa kuchukua maelezo yangu.

“Mmoja aliniambia atanirekodi kwa simu ili nikikimbia wanirushe kwenye vyombo vya habari.

Jilani.

“Nilimwambia sawa tu maana wakati huo nilichowaza ni kumuwahisha mwanangu hospitalini.

“Baada ya kunirekodi, wakati huo mwanangu alikuwa katika hali mbaya sana ndipo wakamchukua wakamkimbiza hospitalini.

“Alipofikishwa aliwekewa dripu na oksijeni. Akiwa kwenye oksijeni aliendelea kuwekewa dripu na ndipo nilipoambiwa mwanangu amekufa.

“Mimi ninachomuoma Rais Magufuli ni haki tu itendeke maana hivyo ndivyo hali ilivyokuwa,” alimalizia kusimulia mama huyo akiwa na uchungu.

MAMA MWENYE NYUMBA

Kwa upande wake, mama mwenye nyumba aliyempangishia chumba mama huyo, Lisa John alisimulia mkasa mzima na kwamba, waliwekwa mahabusu kwa kuonewa kwani siyo yeye aliyeiba simu.

“Nakumbuka yule dada aliyeibiwa simu alikuwa anakunywa nje na mumewe. Sasa huko ndipo simu ilikoibwa.

Mama mwenye nyumba.

“Cha ajabu nilishangaa kusikia ni mama huyu kwani wakati yule dada na mumewe wakinywa baa, huyu mama alikuwa akinyonyesha mwanaye ambaye sasa ni marehemu.

“Nilimsikia mume wa yule dada akimwambia kuwa aachane na huyu mama kwa sababu siyo yeye aliyeiba simu.

“Hata mimi najua siyo huyu mama aliyeiba simu. Tangu tukio hilo litokee (kifo cha mtoto), yule dada aliyempeleka huyu mama polisi alitoweka na mume wangu na hatujui walikoelekea,” alisema mama mwenye nyumba.

SHUHUDA WA TUKIO

Kwa upande wake shuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka kutajwa jina alisema kuwa, wao kama wananchi walicharuka na kutaka mtoto huyo asizikwe hadi haki itendeke.

“Wametubembeleza, tumekubali mtoto azikwe, lakini lazima haki itendeke,” alisema shuhuda huyo wakati mtoto huyo akizikwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

KAMANDA MSANGI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi alikanusha polisi kusababisha kifo cha mtoto huyo.

“Yule mama alipofika nyumbani mtoto wake aliumwa, akampeleka hospitalini na alifia hospitalini.

“Hizi taarifa za kufia mahabusi si za kweli, kwanza hicho kituo hakina mahabusu ya wanawake,” alisema Kamanda Msangi.

Stori: Mwandishi Wetu, Mwanza

VIDEO: FUATILIA KISA HICHO