
MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha na kufunguliwa mashtakata mapya kuhusu kesi ya uchochezi kwa ndoto aliyowahi kuota kuhusu Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Kabla ya tukio hilo, Mahakama ya Wilaya ya Arumeru jijini Arusha mapema leo Aprili 27, 2018 ilimwachia huru Lema katika kesi yake ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili baada ya upande wa mashtaka kushindwa kutoa ushahidi mahakamani.
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amethibitisha hilo na kusema kuwa Lema leo alihudhuria Mahakamani kwa ajili ya kesi iliyokuwa ikimkabili.
“Polisi Arusha wamemkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwa kile kinachodaiwa uchochezi dhidi ya Rais kuhusiana na ndoto aliyowahi kuota. Lema alifika Mahakamani leo kwa ajili ya kesi iliyokua ikimkabili kuhusiana na ndoto alizoota miaka miwili iliyopita. Baada ya Mahakama kufuta kesi hiyo leo na kuachiwa, polisi walimkamata tena na kumfungulia kesi upya kwa mashtaka yale yale,” alisema John Mrema.
Kesi hii ni mwendelezo wa kesi iliyokua ikimkabili Lema na ambayo ilimsotesha Mahabusu (Magereza) kwa zaidi ya miezi muinne kuanzia mwishoni mwa mwa aka 2016 hadi 2017 kabla ya kuachiwa kwa dhamana.