×

Ocean Road Yaondoa Hofu Upimaji wa Tezi Dume

WANAUME wengi wameonyesha wasiwasi wao na zoezi la upimaji wa tezi dume, wengi wakidai kwamba huwa ni wa udhalilishaji jambo ambalo limepingwa na wataalamu wa afya.

 

Ili kujua ukweli, mwandishi wa makala haya ameamua kukuletea kile ambacho amekizungumza Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI). Taasisi hiyo ya Saratani ya Ocean Road imesema upimwaji wa saratani ya tezi dume kituoni hapo hufanyika kwa njia ya damu na si kwa kidole kama ilivyozoeleka.

 

Akizungumza na wanahabari na mwandishi wa makala haya akiwemo wakati wa kuhamasisha matembezi kuhusu uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti, mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Dk. Julius Mwaiselage alisema kipimo hicho hutumika kwa vipindi vya hatua zote za uchunguzi. Anasema huo ni mwongozo ambao umewekwa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na hospitali zote zinaufuata.

 

Akifafanua zaidi Dk. Mwaiselage anasema: “Upimaji huu unafanyika katika hatua za uchunguzi kupitia damu, mwanaume yule ambaye anatakiwa kufanyiwa uchunguzi huo anafika katika hospitali au kituo husika cha afya na anapimwa kwanza kwa kutumia damu kama ilivyo kwa HIV na malaria.”

 

Dk. Mwaiselage anasema baada ya upimaji huo majibu atakayoyapata mpimwaji itategemea kama ana dalili za tezi dume au hana. Anabainisha kuwa iwapo hana dalili atapewa ushauri arudi baada ya miaka miwili na kama anazo dalili zikionekana atakwenda katika vipimo vya ziada lakini havihusiani na kidole kwani navyo pia vinahusisha damu.

 

“Mpaka kufikia hatua za juu zaidi za vipimo ambavyo sasa itathibitika kwamba ni tezi dume, ataendelea na vipimo zaidi vikiwemo vya radiolojia. “Huu upotoshaji wa kwenye mitandao ya kijamii unalenga kutisha watu kutokana na maadili yetu tunashtuka, kwa hatua za juu ni suala la mgonjwa na daktari,” anasema.

Tumelazimika kutoa maelezo haya ya mtaalamu huyu wa saratani kutokana na upotoshwaji unaofanywa kwenye mitandao mbalimbali kwamba upimwaji wa tezi dume hufanyika kwa kutumia kidole, jambo ambalo limekanushwa na daktari huyu aliyebobea na mambo ya saratani ikiwemo hii ya tezi dume. Bila shaka kwa ufafanuzi huu, wanaume sasa wataondoa hofu na kwenda kupimwa afya zao.

 

TEZI DUME NI NINI?

Tezi dume ni sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa kiume. Inaundwa na sehemu mbili, lobes, ambazo zimeunganishwa na kufunikwa kwa nje kwa utando wa tishu. Tezi hii ipo mbele kidogo ya puru (rectum) na chini kidogo ya kibofu cha mkojo. Tezi dume inauzunguka mrija unaounganisha kibofu cha mkojo na uume (urethra). Mojawapo ya kazi za tezi dume ni kutoa majimaji yanayochanganyika na mbegu za kiume (sperms) wakati wa kilele cha tendo la kujamiiana.

 

Kwa kadiri mwanaume anavyozeeka, ni jambo la kawaida pia kwa tezi dume kuongezeka ukubwa na kuvimba. Hali hii kitabibu huitwa Benign Prostate Hyperplasia au wengine hupenda kutumia maneno Benign Prostate Hypertrophy kwa kifupi BPH. Ukuaji wa tezi dume hupitia hatua kuu mbili. Hatua ya kwanza hutokea kipindi cha balehe wakati tezi dume inapoongezeka ukubwa na kuwa mara mbili ya ilivyokuwa hapo awali.

 

Baada ya hapo ukuaji husimama kwa muda mpaka kijana anapofikisha miaka 25 hadi 30 ndipo hatua ya pili ya ukuaji huanza tena.Ukuaji huendelea kwa viwango na kasi tofauti kati ya mtu na mtu na hatimaye kusababisha BPH katika umri wa utu uzima.

 

Wakati tezi dume linapokua na kutanuka, utando wa tishu unaolizunguka hutanuka pia. Hata hivyo, ingawa tezi dume huendelea kukua, hufikia wakati utando wake huacha kutanuka na kufanya tezi dume kubana mrija wa kutolea mkojo kutoka kwenye kibofu. Hali hii husababisha kibofu cha mkojo kuwa na ngozi ngumu na hufanya kibofu cha mkojo kuhisi kutaka kutoa mkojo nje hata kama kiasi cha mkojo ndani yake ni kidogo sana.

 

Hufikia wakati, kibofu huwa dhaifu na kupoteza uwezo wake wa kuhisi kutoa mkojo na hivyo kufanya mtu anapokojoa kushindwa kutoa mkojo wote na badala yake hubakiza kiasi fulani cha mkojo kwenye kibofu. Chanzo halisi cha BPH au vihatarishi vyake (risk factors) havijulikani kwa uhakika. Kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa kuwa BPH hutokea kwa wanaume watu wazima na wazee tu.

STORI: ELVAN STAMBULI