
KUFUATIA baadhi ya wasanii kuugua na kukosa fedha za matibabu na kusababisha kuchangiwa au kusaidiwa na Serikali, staa wa filamu Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ ameiomba Serikali kuwapa wasanii elimu ya uwekezaji.
Dude aliiambia Za Motomoto News kuwa, suala la wasanii kuugua na kushindwa kujilipia gharama za matibabu nje ya nchi limekuwa likimuumiza mno hivyo kuiomba Serikali kuwaboreshea mazingira ya kazi zao na kupatiwa elimu ya uwekezaji kwa hicho kidogo wanakichopata.
“Tunaiomba Serikali ituboreshee mazingira ya kazi zetu maana tunateseka sana hasa pale tunapopatwa na magonjwa yanayohitaji matibabu ya nje ya nchi au hata hapa nchini. Pia tupate elimu ya uwekezaji kwa fedha hizi kidogo tunazopata maana hatuna elimu hiyo pamoja na bima ya afya,” alisema Dude.
Hivi karibuni, mwigizaji mkongwe Bongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ alisafirishwa kwenda nchini India kwa matibabu kwa msaada wa Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe hali ambayo iliibua minong’ono kwani ni msanii ambaye amefanya kazi nyingi na matangazo mengi, lakini alikosa fedha zake mwenyewe kwa ajili ya kumsafirisha nje kwa matibabu.