
ZANZIBAR: Taharuki kubwa imetokea Kisiwani Unguja, Zanzibar juzi katika Bandari ya Malindi ambapo mtu mmoja aliokolewa kutoka ndani ya kontena, analodaiwa kukaa ndani yake kwa siku nne.
Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, walianza kusikia kontena moja likigongwagongwa kwa nguvu huku mtu akipiga kelele za kuomba msaada. Akielezea kwa undani shuhuda Hamisi Ali Hamisi mkazi wa Magomeni, Unguja alikuwa na haya ya kusema:
“Baada ya kusikia sauti ya kontena kugongwa na sauti kwa mbali ya mtu ilibidi tuanze kazi ya kulitafuta kontena hilo ambalo lilikuwa likisikika likigongwa kwani eneo hilo kulikuwa na makontena mengi yaliyopangwa, yakisubiri kupakizwa katika meli.
“Baada ya kazi kubwa, hatimaye vikosi vya uokoaji na askari wa jeshi la polisi pamoja na wa kikosi cha maji, walifanikiwa kulipata kontena hilo ambapo walipolifungua, mwanaume huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 mpaka 30 alitoka huku akionesha kudhoofika, akachukuliwa na jeshi la polisi mpaka kwenye gari dogo lililokuwa eneo hilo na kuondoka naye.
“Yalikuwepo maneno mengi, wengine wakisema alikuwa anatoroka nchi kwenda ng’ambo, wengine walisema ilikuwa ni bahati mbaya tu na kwamba alipitiwa na usingizi
Kamanda wa Polisi wa Mjini Magharibi Kisiwani Unguja, ACP Mkadamu Khamis Mkadamu aliliambia UWAZI kuwa kijana huyo ni mvuvi na kwamba, akiwa katika kazi yake hiyo, mvua kubwa ilianza kunyesha hali iliyomfanya kuingia katika kontena hilo lililokuwa bandarini hapo, lakini baadaye alipitiwa na usingizi.
“Baadaye, wafanyakazi wa bandari, bila kutambua kwamba kuna mtu ndani ya kontena hilo, walilifunga na kwenda kulipanga mahali yanapohifadhiwa makontena, ambapo siku nne baadaye ndipo ilipogundulika kwamba kuna mtu ndani ya kontena hilo, akaokolewa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya kupata huduma ya kwanza,” alisema Kamanda Mkadamu ambaye hata hivyo alishindwa kutaja jina la kijana huyo kwa madai kwamba alikuwa nje ya ofisi yake.
STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI