×

Mambo Haya Ma-5 Yatakupa Yafanikio Makubwa

MPENZI msomaji karibu jamvini tuendelee kupeana mbinu mbalimbali za kupata mafanikio maishani endapo tu tutazingatia mafundisho haya. Kumbuka wapo wengi waliokombolewa na ukurasa huu ambao mara zote hutuma shukurani zao nyingi.

Nianze kwa kukukumbusha tu kwamba, hivi unakumbuka Mwaka 2018 ulipokuwa unaanza? Mara nyingi mwaka unapoanza kila mtu huwa anakuwa na hamasa ya kufanya jambo kubwa katika maisha yake kwa mwaka husika. Watu huwa na orodha ndefu na nzuri ya mambo gani ambayo wanakusudia kuyafanya.

Kila mtu ifikapo Januari huona kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kufanikiwa na kutimiza malengo aliyonayo katika maisha yake hadi ifikapo Desemba.

Lakini cha kushangaza, miezi michache baadaye, wengi hujikuta hawana ile hamasa tena ya kusonga mbele kama ambavyo walianza awali.

Na hii husababisha wengi kukata tamaa mapema kabla hata hawajafanikiwa kutimiza lengo hata moja la mwaka.

Inawezekana na wewe unapitia kipindi kama hiki baada ya kuweka mipango yako tayari ya namna ambavyo ulitamani ufanikiwe kwa mwaka huu ukiwa na hamasa ya hali ya juu.

Hata hivyo, kuna mambo ambayo huwezi kufanikiwa hata kidogo kama hutarekebisha baadhi ya vitu kwenye maisha yako.

Katika kufuatilia watu waliofanikiwa na kufundisha kuhusu mafanikio, nimegundua mambo matano (5) ambayo kila anayetaka kufanikiwa ni lazima aamue kuachana nayo ili aongeze uwezekano wa kufikia malengo makubwa zaidi.

Hii ni kwa sababu kama utaendelea kuishi kwa mazoea, ukiwa na tabia zilezile na kufanya mambo yaleyale, kwa uamuzi uleule, basi utajikuta unapata matokeo yaleyale na hakutakuwa na mabadiliko yoyote yale katika maisha yako;

1: MWELEKEO

Jambo la kwanza unalopaswa kufanya ni kuachana kabisa na maisha yasiyo na mwelekeo. Kumbuka siku zote kuwa mwelekeo ni muhimu kuliko kasi yako. Watu wengi sana wanaonekana wako kasi na maisha yao ila hawana mwelekeo. Ni lazima uamue kabisa kuwa unataka jambo gani kwa umahsusi wake. Usiende tu bila mwelekeo kuhusu kazi, biashara yako, uwekezaji, masomo na mengineyo.

Ndugu yangu jitahidi sana kutengeneza ramani ya maisha yako kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa kumi na mbili. Kwa kila jambo, liwekee mkakati maalum wa namna ya kulifanikisha na kila siku ujue unataka kufanikiwa kwenye nini.

Kama kweli umedhamiria kufanikiwa, achana na ile tabia ya kujaribu kufanya kitu kipya kila baada ya muda mfupi na mwisho wa siku unajikuta hakuna chochote cha maana ambacho umefanikiwa kukifanya. Jiulize tena leo, mwelekeo wa maisha yako ni upi? Usikubali kwenda tu bila mwelekeo kwani ukienda hivyo, kufeli kwako ni lazima!

2: MUDA

Mara zote nimekuwa nikifundisha kuwa, lazima uachane na tabia ya kupoteza muda katika ratiba zako za kila siku. Kati ya rasilimali muhimu sana katika maisha yako ni muda. Hii hutokana na jinsi unavyotumia muda wako ambao ndiyo utakujulisha kama unapiga hatua au la. Muda ukishapotea huwezi kurudi tena. Usikubali kuwa mtu ambaye unapoteza muda wako kwa mambo ambayo siyo ya msingi kwenye maisha yako. Amua na kuapa kuwa, kuanzia leo utakuwa mtu unayetunza muda wako vizuri.

Rafiki usipoteze muda wako kwa kupiga stori zisizojenga, usipoteze muda wako kwa kuangalia sinema au kukaa vijiweni kila wakati huku ukiwa huna nafasi ya kujisomea vitabu vya kukusaidia kutimiza ndoto zako. Usipoteze muda wako kulala kwa saa kumi kwa siku wakati ungeweza kutumia sehemu ya muda huo kufanya shughuli za kujiongezea kipato. Achana na tabia ya kupoteza muda. Amua kuwa mtu unayejali muda wako. Kila wakati jiulize; ‘Hivi haya ni matumizi sahihi ya muda wangu?’

3: MSIMAMO

Kama kweli una shauku ya mafanikio, achana na tabia ya kuendeshwa na misisimko ya maisha ambayo inakutoa kwenye malengo yako. Ili ufanikiwe ni lazima uamue kuwa na mtazamo thabiti katika kile ambacho umeamua kukifanya. Bila hivyo, utakuwa ni mtu wa kutoka kwenye mstari kila wakati. Moja ya vitu ambavyo huwa vinawaharibia watu wengi mwelekeo katika maisha yao ni ile hali ya kufanya mambo kwa msisimko bila kujipanga.

Kuna baadhi ya watu huwa wakisikia kuna biashara au kilimo fulani kinalipa, basi wanachukua hela zao zote na kujiingiza kwenye biashara hiyo. Matokeo yake hujikuta wanapoteza kila kitu.

Siku zote kumbuka huna uwezo wa kufanya kila kitu na si kila mtu anaweza kufanikiwa katika kila kitu ambacho mwingine anafanya au amefanikiwa. Amua leo kuwa mtu ambaye hutaendeshwa na msisimko wa yale wengine wanayosema na badala yake utajikita katika kutekeleza malengo yako bila kutolewa nje ya mstari. Msisimko utakuja ila amua kuachana nao kisha jikite kwenye ulichoamua kukifanya.

4: MARAFIKI

Jambo la nne unalopaswa kuwa makini nalo ni kuachana na marafiki ambao wanarudisha nyuma maendeleo yako. Marafiki zako wana uwezo mkubwa wa kukufanya usonge mbele au urudi nyuma. Ukitafakari maisha yako, utakuwa ni shahidi kuwa kuna baadhi ya marafiki zako wengi ambao wamekuwa sababu ya wewe kuingia katika matatizo ya kibiashara, kifedha, kihusiano na wengi ambao walikushauri vibaya na ikakusababishia kujikuta katika wakati mgumu. Ni muhimu sana kuamua kufanya ukaguzi wa mtandao wako wa marafiki na ujiulize wale ambao wamekuwa msaada uendelee nao na wale ambao wamekuwa hawana msaada uachane nao au upunguze ukaribu nao.

Huu pia ndiyo wakati mzuri wa kujaribu kuangalia aina mpya ya marafiki ambao unatakiwa uwe nao katika maisha yako ili uweze kufikia malengo yako. Ni vigumu mno kupata matokeo makubwa zaidi ya yale uliyonayo kama utaendelea na aina ileile ya marafiki bila kuwabadilisha kabisa. Amua kuachana na marafiki wanaokatisha tamaa, wanaokushauri vibaya na ambao wanakuingiza katika matatizo.

5: BAJETI

Rafiki yangu katika maisha haya, acha kuishi bila bajeti. Kati ya sababu zinazoweza kukuingiza kwenye matatizo ya kipesa ni hali ya kuishi bila kuwa na bajeti maalum ya kutumia pesa zako. Hii ndiyo husababisha watu wengi waingie kwenye madeni na huwafanya kuishi juu ya uwezo wao wa kile wanachoingiza.

Kaa chini na upange bajeti yako ya kila mwezi, jinsi utakavyoingiza na vile utakavyotumia. Jitahidi sana usiishi juu ya kile unachoingiza kwa mwezi. Ukiweka bajeti yako na ukagundua kuwa matumizi yamekuwa makubwa kuliko kipato, basi angalia namna unavyoweza kupunguza gharama za matumizi yako ili kwa namna yoyote ile, usijiingize katika madeni yasiyo ya ulazima kwenye maisha yako.

Leo naishia hapa, lakini tukutane wiki ijayo kwa mjadala mwingine.