×

FARAJA NYAL ANDU; MKOMBOZI WA ELIMU KUPITIA MTANDAO

Faraja Kotta Nyalandu,

NAMPENDA Faraja. Naota kuwa kama yeye na nifike mahali alipo. Niisaidie jamii na niheshimike, niwe mke na mama bora.

Hayo yanaweza kuwa mawazo ya wanadada wengi mitaani ambao wanamfahamu mwanadada huyu wa chuma, Faraja Kotta Nyalandu, mwenye mchango mkubwa katika jamii ya Kitanzania hasa kwenye suala zima la elimu.

Lakini wengi inawezekana kabisa wakawa wanaota ndoto nzuri, wana maono mazuri na wanahitaji kufika mahali fulani kwenye maisha yao, lakini wakawa hawafahamu namna ya kufikia ndoto zao hizo au wanafahamu, lakini hawathubutu!

Sasa, ili kufikia ndoto zako, Faraja anasema: “Kwanza kabisa ni lazima uwe na ndoto, ufahamu namna ambavyo unaweza kufikia ndoto zako na uthubutu.“Watu wengi wameishia kuota, lakini hawakuweza kuthubutu, ndoto zao zikakosa maana.”

Faraja aliwahi kuyasema maneno hayo kupitia Kipindi cha Mkasi akihojiwa na mtangazaji Salama Jabir. Lakini mbali na maneno hayo mazuri, ukiingia kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram, mbali na jina lake, maandishi ya mwanzo kabisa kukutana nayo ni “We can DREAM, we can BE, we can PROSPER!

Yakiwa na maana kwamba, “Tunaweza KUOTA, tunaweza KUWA, tunaweza KUNUFAIKA! Kwa namna moja au nyingine tunaweza kusema kwamba, hivyo ndivyo Faraha anavyoamini, kwamba inawezekana kwa kila mmoja.

FARAJA NI NANI?

Wengi wanaweza kuwa wanamfahamu na wengi wanaweza kuwa hawamfahamu pia. Lakini kama humfahamu, lisiwe suala la kukuumiza kichwa.

Ni hivi; Faraja ni mwanadada wa Kitanzania, aliyezaliwa na kukulia jijini Dar. Aliwahi kuwa Miss Ubungo, baadaye Miss Kinodoni na hiyo ilikuwa ni kabla ya kuibuka kidedea kwenye kinyang’anyiro cha Miss Tanzania mwaka 2004.

Zaidi, Faraja ni mke wa mwanasiasa maarufu nchini, Lazaro Nyalandu na ni mama wa watoto wawili! Hapo vipi? Bila shaka umemfahamu kidogo.

MCHANGO WAKE KATIKA JAMII NI UPI?

Nimeeleza hapo awali kwamba, Faraja ambaye ni mwanasheria na mwandishi wa vitabu, ameandika kitabu kiitwacho Unaweza; Mbinu Kumi za Kumudu Masomo Yako, mchango wake mkubwa kwenye jamii ni katika elimu.

Ndiyo, inawezekana akawa na mchango kwenye mambo mengine mengi tangu akiwa Miss Tanzania, kamishna wa masuala yanayohusu ugonjwa wa Ukimwi, kushirikiana na taasisi za vijana na mambo mengine mengi, lakini kinachomtambulisha zaidi kwa sasa ni huduma ya elimu kupitia ‘platifomu’ yake ya Shule Direct ambayo inashirikiana kwa ukaribu na wizara ya Elimu.

Hii ni platifomu ambayo inawawezesha wanafunzi kujisomea vitabu na kuingia kwenye mijadala mbalimbali na wanafunzi wenzao ambao wapo sehemu tofautitofauti ndani ya nchi!

ILIKUWAJE AKAANZISHA PLATIFOMU HII?

Swali zuri. Jibu lake ni kwamba, mwanadada huyu wa chuma, amewahi kuweka wazi kwamba wazo la kuanzisha platifomu hii alilipata wakati akiwa masomoni Uingereza. Msikie mwenyewe;

“Nilipokuwa masomoni Uingereza, nilikuwa mama mwenye watoto wadogo wawili ambao walikuwa wanahitaji uangalizi wangu wa karibu zaidi. Kutokana na hali hiyo, sikuwa na muda mwingi wa kuwa darasani kama wanafunzi wengine, ambapo wakati ambao nilikuwa ninakwenda darasani ilinilazimu kuchukua rundo la vitabu maktaba kwa ajili ya kujisomea.

“Lakini baadaye niliweza kugundua kwamba njia hiyo ilikuwa ngumu ya kusoma kupitia mtandao ndiyo ilikuwa rahisi zaidi. Nilipoamua kuifanyia kazi ndiyo nikaona ni rahisi zaidi maana nilikuwa nina uwezo wa kusoma nakala na vitabu vingi kwa muda mchache.

“Hapo ndipo nilipofikiria kuhusu wadogo zangu na ndugu zangu wa Tanzania kwamba wanaweza kuitumia njia hiyo pia kuweza kusoma na ikawanufaisha zaidi.”

Faraja anasema alifikiria hivyo kwa sababu baada ya kuigundua njia hiyo, alifahamu kwamba Tanzania bado tuna upungufu wa namna ya wanafunzi kusoma. Tuna njia chache. Ambazo ni kuwa darasani na kumsikiliza mwalimu, kusoma masomo ya ziada kwa wanaomudu au kwenda maktaba na kukusanya vitabu kwa ajili ya kusoma.

Njia ya kusoma na kujadili mambo mbalimbali kuhusu masomo kupitia mtandao, wengi hawaifahamu au hawajui umuhimu wake na hata inavyoweza kuokoa muda. Hapo ndipo mawazo ya kuanzisha Shule Direct yaliweza kuzaliwa.

AMEFANIKIWA KWA KIASI GANI?

Kupitia Shule Direct, Faraja ameweza kuwafikia mamilioni ya wanafunzi ndani na nje ya Tanzania na malengo yake ni kuhakikisha kila mwanafunzi nchini anapata elimu bora.Huyo ndiye Faraja. Hata wewe unaweza kuwa na ndoto zako na ukatimiza kama yeye.

Makala: Boniphace Ngumije