
Mwanamuziki wa Bongo Fleva Frida Amani akiongea wakati wa mjadala uliondaliwa na taasisi ya Columbia Global Centers kwa wanamuziki wa Tanzania. Kushoto ni msanii Emmanuel Simwinga maarufu kama IzzoBusiness.

SHIRIKA la Columbia Global Centers imeandaa mjadala ambao umeleta pamoja wasanii wa Tanzania kuzungumzia jinsi wanavyoweza kutumia vipaji vyao na kazi zao kuendeleza miradi ya jamii.
Mjadala huo umefanyika jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mhadhiri wa Chuo Cha Columbia University Prof Yogi Trived.
Akizungumza kwenye mjadala huo, Prof Trived alisema kuwa muziki unaleta watu wa aina zote, rika na rangi na kwa hivyo ukitumika vizuri unaweza kusaidia kuendeleza miradi ya jamii kwa mafanikio zaidi.
Hakuna mtu ambaye hapendi muziki na muziki unatokana na juhudi za wasanii wetu. Ni muhimu kwa wasanii wakatambua kuwa kazi yao sio kusimama kwenye majukwaa na kutumbuiza. Ni zaidi ya hivyo. Wasanii wanao uwezo wa kuchangia na kuhamashisha miradi mbali mbali ya Jamii. Alisema Trived huku akiongeza kuwa serikali inatambua umuhimu na mchango wa wasanii kwenye jamii na kuwatumia kwenye kufanikisha Maendeleo ya jamii.
Baadhi ya wasanii ambao walikuwepo ni pamoja na Frida Amani, Rosery Robert maarufu kama Rosa Ree, Webiro Wassira maarufu kama Wakazi, Emmanuel Simwinga maarufu kama IzzoBusiness na Malaika.
Akichangia kwenye mjadala huo, msanii Webiro Wassira alitoa changamoto kwa wasanii wenzake kujitambua na kujiamini kuwa wanao uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo katika jamii. Natoa mfano kwa upande wangu. Nimeshiriki kwenye kampeni ya Kili Project ambao imekuwa ni mahususi katika kupanda miti ili kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa.
‘Hii kampeini ilikuwa ni maalum katika upandaji miti kwenye maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro. Na si kupanda miti, bali tulienda zaidi kuhamamisha jamii katika utunzaji wa miti iliyopo na zaidi ile ya asili. Kampeini hii ilikuwa na mafanikio sana na kwa hivyo natoa wito kwa serikali na mashirika mbali mbali kutambua uwezo tulionao sisi wasanii na kutumia kwenye miradi yao ya kijamii.
Kwa upande wake, msanii Malaika ambaye ni balozi wa sickle cell alisema kuwa mbali na wasanii kuwa kioo cha jamii lakini ni vizuri kuwa na ushirikiano kwa wasanii wenyewe. ‘Kwanza wasanii sisi lazima tuwe na ushirikiano, lakini zaidi kwa vyombo vya habari kuwa karibu na kufanya kazi na wasanii kwa maendeleo zaidi.