The House of Favourite Newspapers

BABA DIMPOZ AMLIPUA BABA DIAMOND

Faraji Nyembo

DAR ES SALAAM: HII ni vita ya wakubwa! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya baba wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, Faraji Nyembo kumlipua baba wa Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Abdul Jumaa kutokana na tabia ya kumsema mwanaye huyo vibaya.

Baba Dimpoz alifunguka hayo juzi katika mahojiano maalum kwa njia ya simu na Risasi Mchanganyiko kuhusu ugonjwa wa mwanaye, ambaye yupo Afrika Kusini kwa matibabu.

Awali, mzazi huyo mwenye maskani yake mjini Tabora alianza kwa kusema, anamshukuru Mungu mwanaye anaendelea vyema baada ya kufanyiwa upasuaji wa koo hivi karibuni.

 

AUZUNGUMZIA UGONJWA WA MWANAYE

Akielezea kuhusu ugonjwa wa mwanaye, baba Dimpoz alisema Dimpoz alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kuota nyama kwenye koo kwa muda mrefu lakini anamshukuru Mungu kwani baada ya kufanyia upasuaji alikaa siku mbili kwenye chumba cha uangalizi maalum ‘ICU’ lakini kwa sasa anaendelea vizuri.

 

ATOBOA SIRI YA UGONJWA

Aliendelea kusema kwamba ugonjwa huo umewahi kumpata hata mwanaye mwingine ambaye ni dada wa Dimpoz ambapo alifanyiwa upasuaji akapona.

“Huu ugonjwa si kwa Dimpoz tu hata dada yake naye aliwahi kuugua lakini tunashukuru alitibiwa kwa upasuaji akapona,” alisema baba Dimpoz.

 

AMUOMBEA APONE HARAKA

Akizidi kuzungumza na Risasi Mchanganyiko, baba Dimpoz alisema licha ya kutopata msaada wowote kutoka kwa mwanaye huyo lakini anamuombea apone haraka arudi kwenye majukumu yake ya kila siku.

“Hata kama mwanangu hanisaidii chochote siwezi kumnenea mabaya au kumlalamikia bali namuombea apone aendelee na majukumu yake kama kawaida naamini ipo siku Mungu atamleta kunisaidia,” alisema baba Dimpoz.

AMLIPUA BABA DIAMOND

Baada ya kumaliza hayo ya ugonjwa wa mwanaye, baba Dimpoz alitumia fursa hiyohiyo kumchana baba Diamond akidai kuwa amekuwa akimnenea mabaya mwanaye (Diamond) pindi anapokosea.

“Unajua mimi ni mzazi wa tofauti sana, siwezi kumlalamikia au kumsemea mabaya mwanangu kwenye vyombo vya habari kama anavyofanya baba Diamond, ninachofanya huwa namuombea mwanangu awe na maisha mazuri maana nikimuombea mabaya anaweza kupoteza dira ya maisha yake nitakuwa nimefaidika na nini.

“Nilimuona baba Diamond akizungumza kwenye kipindi kimoja cha runinga akimlaumu mwanaye huyo na kumlalamikia kwamba hamsaidii nikamshangaa sana kwa kweli maana siyo tabia nzuri.

 

AMPA USHAURI WA BURE

“Namshauri baba Diamond awe anamuombea mwanaye mafanikio, aungane naye wawe kitu kimoja, afurahie mafanikio yake ipo siku Mungu atamrudisha kwake amsaidie na siyo kumzungumzia maneno ya kumlaani na kumlalamikia kila siku.

“Aige mfano wangu maana mimi huwa simlazimishi mtoto anisaidie bali huwa napambana na hali yangu kwa kufanya kazi kwa bidii na ninampenda sana mwanangu Dimpoz na siwezi kumlaani au kumlaumu maana jina nililompa la Omary ni la baba yangu inakuwaje sasa nimlaani ni sawa na kumlaani baba yangu,” alisema baba Dimpoz.

 

BABA DIAMOND AJIBU MAPIGO

Ili kuleta usawa wa habari, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta baba Diamond ambapo alijibu mapigo na kutoa povu la aina yake akimtaka baba Dimpoz akae kimya na asifuatilie maisha yake.

“Sitaki shobo, huyo baba Dimpoz simfahamu kama hana la kuongea anyamaze, amzungumzie mwanaye hata kama niliongea kuhusu Diamond si mtoto wangu yeye inamuhusu nini?

“Kuhusu huyo Diamond sihitaji kuzungumza chochote kuhusu yeye wala watoto wangu maana hawana faida yoyote kwangu kwa sasa,” alisema baba Diamond.

 

TUJIKUMBUSHE

Katika mahojiano mbalimbali aliyoyafanya baba Diamond na Magazeti Pendwa, amekuwa akimshushia lawama Diamond kwa kudai anashindwa kumsaidia hususan katika tatizo lake la miguu linalomsumbua kwa muda mrefu ilihali ana ‘mkwanja’ wa kutosha.

Jambo hilo limesababisha mara kadhaa mzee huyo amtamkie mwanaye maneno mabaya japo kuna wakati waliwahi kumaliza tofauti zao lakini hadi sasa bado ‘hawaivi’ kivile.

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko.

Comments are closed.