
MARA baada ya Baba Mtakatifu Francisco kumteua Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza,kuwa askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Kuu la Dar es Salaam, baadhi ya mapadri wamefunguka juu ya utendaji kazi wake.
Wakizungumza na Gazeti la Risasi Jumamosi mapadri hao akiwemo ambaye ameachana na huduma hiyo, Padri Privatus Karugendo, wamemtaja Askofu Ruwaichi kuwa ni mtu ambaye atalisaidia Kanisa Katoliki.
“Ni mtu ambaye ana akili nyingi na ana nadhiri ya ufukara na pia ana msimamo wa kati, si mliberali au conservative (asiyekubali mabadiliko),” alisema Karugendo.
Alifafanua kuwa askofu huyo ana mawazo ya kisasa ukilinganisha na Polycarp Kadinali Pengo ambaye atamuachia ofisi.
Hata hivyo, Karugendo alionyesha wasiwasi wake kuhusu dhana inayojengeka sasa mitandaoni kwamba Kanisa Katoliki linashikwa na watu wa Kaskazini.
“Hii dhana ni potofu na ni ya kuendekeza ukabila, inapaswa kuachwa mara moja. Askofu Ruwaichi ni mtu anayesikiliza watu na hawezi kuwa mtu wa kikabila kama baadhi ya watu wanavyodhani,” alisema.

Naye padri mwingine ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji alisema anavyomjua Askofu Ruwaichi anaamini kwamba atalisukuma mbele Kanisa Katoliki.
“Atalisaidia kanisa kuliko mzee (Pengo) kwa sababu huyu ni mtu anayesikiliza watu na kuchambua anachoambiwa,” alisema padri huyo huku akisisitiza kwamba anaamini uteuzi huo umezingatia weledi wa askofu huyo.
Naye padri mwingine wa jijini Dar alipoulizwa maoni yake juu ya uteuzi huo alisema kifupi kwamba uteuzi huo ni sahihi na hana wasiwasi na utendaji wa Askofu Ruwaichi.Kabla ya uteuzi huu, Askofu Ruwaichi alikuwa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza.
Askofu Mkuu Ruwaichi alizaliwa tarehe 30 Januari 1954, Mulo, Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 25 Novemba 1981. Tarehe 9 Februari 1999 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu na kuwekwa wakfu tarehe 16 Mei 1999.
Tarehe 15 Januari 2005, Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na kusimikwa rasmi tarehe 19 Februari 2005. Tarehe 10 Novemba 2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza na kusimikwa rasmi tarehe 9 Januari 2011.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo ambaye atamuachia uongozi wa jimbo Askofu Ruwaichi, aliwahi kuwaambia waumini wa kanisa hilo Oktoba 2014 kuwa hawana sababu ya kuingiwa wasiwasi kuhusu hali yake kiafya kwa kuwa angestaafu miaka mitano ijayo.

Akihubiri katika ibada maalumu ya misa iliyoandaliwa na Utume wa Wanaume Katoliki (Uwaka) jimboni humo mwaka huo, Kardinali Pengo alieleza kuwa anajiandaa kustaafu kisheria, jambo ambalo halina sababu ya kuwaweka roho juu waumini.
Katika mahubiri yake ya muda mfupi kwenye misa hiyo iliyofanyika Kituo cha Kiroho Mbagala, Dar es Salaam Kardinali Pengo alitumia muda huo kuzungumzia afya yake, akisema kwa muda sasa amekuwa haonekani hadharani kutokana na kuumwa.Hata hivyo, hakutaja aina ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.
STORI: Elvan Stambuli, DAR