TANZANIA imewekwa kwenye orodha ya nchi sita zilizo hatarini kupatwa ugonjwa hatari wa Ebola. Hii baada ya kutolewa ripoti ya tatu inayohusu ugonjwa huo katika nchi zinazopakana na Kongo DR ambapo tayari kumeripotiwa kuwepo ugonjwa huo.
“Tupo kwenye hatari ya kupatwa ugonjwa wa ebola kutokana na muingiliano mkubwa uliopo kati ya nchi ya Congo na nchi yetu ya Tanzania. Tumekuwa kundi la pili miongoni mwa nchi sita kutoka nchi zilizo katika hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo.
“Ebola bado haijaingia rasmi Tanzania, lakini tumejipanga endapo itaingia wananchi wetu wasiweze kupata madhara. Tumeunda timu kwa watu waliokaribu na maeneo hatarishi, tumeshaandaa vituo kwa ajili ya wagonjwa wa ebola endapo watabainika wapelekwe wapi.

“Tunatoa taarifa rasmi kuwa tuna wagonjwa 4 waliogundulika wana vimelea vya homa ya Chikungunya hadi sasa kwa Dar es Salaam, waliothibitika kuwa na homa ya Dengue ni 226. Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Dar, zipo hatarini kupata Dengue na Chikungunya,”” amesema Waziri wa Afya, Dkt. Ummy Mwalimu.
Dkt. Ummy amewataka wananchi kuchukua tahadhari za ugonjwa huo mapema ikiwemo kuepuka kugusan na watu watakaoonekana wana dalili za ugonjwa. Hata hivyo, mpaka sasa hakuna mtu aliyeripotiwa kuambukizwa ugonjwa huo nchini.
Hivi karibuni serikali ilifunga mtambo maalum katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar ambao utakuwa unapima na kubaini viashiria vya ugonjwa huo kwa wageni wanaongia nchini.