


BENKI ya NMB imeamua kuanza kutoa elimu kwa wazazi wenye watoto kuanzia wadogo hadi wenye umri wa miaka 13 ili wawe na uelewa wa kutosha na kufahamu umuhimu wa kuwawekea akiba.
Hayo yalisemwa na meneja wa Uwajibikaji kwa Jamii wa NMB, Lilian Kisambala, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema benki hiyo inawajali sana watoto na imeona ni bora kutoa elimu ya kutosha kwa wazazi ili wawe na moyo wa kuwafungulia akaunti watoto wao kwa maisha ya baadaye.
Alisisitiza kuwa kwa vile wiki iliyopita ilikuwa Siku ya Mtoto wa Afrika, wakaona ni vyema watumie siku hiyo kuwahamasisha wazazi kuwafungulia watoto wao akaunti katika benki hiyo.
Ni wajibu wa wazazi au walezi kuwaendeleza watoto na kuwa chachu ya mafanikio yao kwa mifano madhubuti. Katika kuthibitisha hilo, wafanyakazi wa NMB wamepata fursa ya kuwapeleka watoto wao kutembelea ofisi zao, kuwaonyesha mazingira, kuwapa elimu mbalimbali na kuwafanya watoto kutambua mahali wanapofanyia kazi.